Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSMA yakarabati bustani Timbuktu na sasa wakulima na wachuuzi wamenufaika

Soko la wazi nchini Mali
MINUSMA/Gema Cortes
Soko la wazi nchini Mali

MINUSMA yakarabati bustani Timbuktu na sasa wakulima na wachuuzi wamenufaika

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Mali, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSMA baada ya kuona athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwenye mbinu za kujipatia kipato miongoni mwa wakulima wa eneo la Timbuktu, uliibuka na mradi wa kuboresha bustani yao ya soko la mboga na sasa nuru ya kujipatia kipato imeonekana.
 

Bustani hii ya Tarabangou iliyoko mji wa Timbuktu jimboni Timbuktu nchini Mali inafananishwa na mapafu ya uchumi wa jamii ya eneo hili, na alama ya mnepo kwa uwezo wake wa kuepusha mizozano baina ya jamii.

Alhad Ag Aldjoumagat ni Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Tarabangou na anasema «kutokana na mzozo unaoendelea, hatukuwa na la kufanya na hakuna mtu alitusaidia. Lakini baada ya maeneo ya kaskazini kutwaliwa tena, MINUSMA imetusaidia kwa kuweka paneli za sola, ukarabati wa bwawa, na kuunda chama cha ushirika. »

Bustani hiyo ya mboga za kuuza sokoni ina ukubwa wa hekari 30 na wanaushirika 374 wanawake kwa wanaume sasa wameanza tena kupanda mboga za majani, viazi, vitunguu na hata nyanya, hali ambayo inawezesha sasa kupata fursa za ajira na kipato.

Kwa mujibu wa Alhad, bustani yao iliyokarabatiwa kwa zaidi ya dola Elfu Tisini, imekuwa mfano kwa kuwa wanapata ugeni mara kwa mara kujifunza kile ambacho wao wameweza kufanikiwa.

Wachuuzi wa mboga na matunda kama vile Talhmitt Walet Alidji wananufaika na bustani hii kwa kuwa wanapata pia maji safi ya kusafisha mboga kabla ya kuzipeleka sokoni akisema, « tunafika hapa saa mbili asubuhi, na majira ya saa tano au saa sita mchana tunaelekea mjini Tunanunua mboga na matunda na kisha tunaenda kuuza mjini. Tunauza mboga, viazi, maharagwe na matunda. Ni kazi ngumu kwetu lakini pia kwa wakulima. Tunatembea kilometa kadhaa kabla ya kupata gari la kutufikisha mjini. Msaada wa MINUSMA umekuwa na faida pia kwetu kwa sababu awali, shughuli zilimalizika tu baada ya mavuno. Lakini kwa msaada wa MINUSMA shughuli zinaendelea hata wakati wa msimu wa mwambo. Hii inatusaidia kukimu mahitaji yetu."