Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio lingine Mali dhidi ya walinda amani; 2 wauawa

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Shambulio lingine Mali dhidi ya walinda amani; 2 wauawa

Amani na Usalama

Nchini Mali, walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja huo wa kulinda amani nchini humo, MINUSMA, wameuawa leo asubuhi kwenye mji wa Douentza ulioko mkoa wa Mopti kaskazini-mashariki mwa mji mkuu Bamako.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani kuwa walinda amani hao wamepoteza maisha baada ya kifaru walimokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi.

Amesema walinda amani wengine wawili walijeruhiwa katika tukio hilo na tayari walinda amani wengine MINUSMA wameimarisha usalama kwenye eneo hilo wakati huu ambapo taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zinaendelea kukusanywa.

“Hili ni tukio la sita ambapo msafara wa MINUSMA umeshambuliwa tangu tarehe 22 mwezi uliopita wa Mei. Na ni tukio la pili ambapo walinda amani wanapoteza maisha katika wiki moja,” amesema Bwana Dujarric.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani shambulio hili la leo dhidi ya walinda amani, “ambao kama mjuavyo wanatekeleza majukumu yao nchini Mali katika mazingira magumu kupitia maagizo kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ,” amesema Dujarric huku akiongeza kuwa Guterres pia amewatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Wakati huo huo, Mkuu wa MINUSMA, El-Ghassim Wane, amelaani shambulio hilo sambamba na lile lilitokea mkoa wa Kayes, mapema wiki hii ambapo watendaji wawili wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Mali waliuawa.

Pamoja na changamoto za usalama zinazokumba walinda amani, Bwana Dujarric amesema katika mkoa wa Kidal, walinda amani wametoa huduma mbalimbali za msaada kwa raia wa miji ya Anefis na Tanbankort kama sehemu ya harakati zao za kusaidia wananchi wa maeneo ya kaskazini mwa Mali.