Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kauli zao kuhusu mashambulizi nchini Ukraine

Bibi raia wa Ukraine akiwa na kitukuu chake kutoka Odessa wakiwa katika makazi ya muda ya wakimbizi huko Romania
© UNICEF/Ioana Moldovan
Bibi raia wa Ukraine akiwa na kitukuu chake kutoka Odessa wakiwa katika makazi ya muda ya wakimbizi huko Romania

Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Kauli zao kuhusu mashambulizi nchini Ukraine

Wahamiaji na Wakimbizi

Ikiwa ni wiki moja tangu kuanza kwa mgogoro wa Ukraine kushambuliwa na Urusi, mashirika mbalimali ya Umoja wa Mataifa yamepaza sauti kulaani kinachoendelea nchini humo na kuhimiza hatua za haraka zichukuliwe katika kukomesha machafuko.

IOM walaani ubaguzi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM António Vitorino ameeleza wasiwasi wake kuhusu ripoti za kuaminika za ubaguzi, ghasia na chuki dhidi ya wageni waliokuwa wakiishi Ukraine na sasa wanaondoka nchini huko kukimbia mzozo unaoendelea.

“Niseme wazi, ubaguzi kwa misingi ya rangi, kabila, utaifa au hali ya uhamiaji haukubaliki. Ninachukia vitendo kama hivyo na kutoa wito kwa mataifa kuchunguza suala hili na kulishughulikia mara moja. Wanaume, wanawake na watoto kutoka mataifa kadhaa, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wahamiaji na wanafunzi wanaoishi Ukraine wanakabiliwa na changamoto kubwa wanapojaribu kuondoka katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, kuvuka mipaka na kuingia nchi jirani na kutafuta usaidizi wa kuokoa maisha yao.”

Mkuu huyo wa IOM amezikumbusha nchi Jirani na Ukraine zinahitaji kuhakikisha kwamba wale wote wanaokimbia machafuko, wanapaswa kupewa hifdhi bila vikwazo vya eneo na bila kujali hali zao kwa mujibu wa Sheria ya Kimataifa ya Kibinadamu. Kuwapatia ulinzi na usaidizi wa haraka kutolewe kwa njia isiyo ya kibaguzi na inayofaa kitamaduni, kulingana na sharti la kibinadamu, kwa watu wote walioathiriwa na migogoro katika safari yao ya kusaka usalama.

Wakimizi wa Ukraine wakiwa na watoto kumi na moja wakiingia Romania katika mpaka wa Isaccea
© UNICEF/Ioana Moldovan
Wakimizi wa Ukraine wakiwa na watoto kumi na moja wakiingia Romania katika mpaka wa Isaccea

Kauli ya Mtaalamu Maalum wa UN kuhusu ubaguzi wa Kisiasa na Rangi

Tendayi Achiume ni mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu aina za kisasa za ubaguzi wa rangi, ambaye naye katika taarifa yake kwa vyombo ya habari ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu vitisho vya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni, dhidi ya watu wasio wazungu wanaokimbia Ukraine.  

“Ninaungana na wataalam wengine huru kulaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine, na ninahimiza hatua za haraka zichukuliwe kulinda mamilioni waliolazimika kukimbia mashambulizi yanayoendelea. Tangu mzozo uanze, Waafrika Weusi, raia wa India, raia wa Pakistani, watu wa asili ya Mashariki ya Kati na wengine wametuma ripoti za dharura za matukio ya kutishia maisha, ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni wanapojaribu kukimbia ghasia nchini Ukraine.”

Wakimbizi kutoka Ukraine wakipatiwa chakula baada ya kuvuka mpaka na kuingia Poland mpakani Medyka
© UNHCR/Valerio Muscella
Wakimbizi kutoka Ukraine wakipatiwa chakula baada ya kuvuka mpaka na kuingia Poland mpakani Medyka

Simulizi za manyanyaso kwa wanaokimbia Ukraine

Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa baadhi ya watu wanaripoti kunyimwa malazi katika makazi yakujificha na mabomu ndani ya Ukraine, wengine wanaripoti walinzi wa mipakani kuwazuia kuvuka mpaka au kuwasukuma nyuma ya foleni na hivyo kukosa usafiri ambao ungewaruhusu kupita salama nje ya nchi hiyo na wakati mwingine, wanaripoti kunyimwa kuwasiliana na balozi za nchi zao za asili katika nchi jirani.

Wengi ikiwa ni pamoja na watoto wachanga wanalazimika kusubiri kwa muda mrefu katika maeneo yenye baridi kali bila ya kuwa na makazi. Katika visa hivi vyote, watu hawa na vikundi vinatengwa kibaguzi kwasababu ya rangi zao, kikabila na kitaifa ambao hauruhusiwi kwa mujibu wa sheria za kimataifa, hata katika mazingira ya vita.

Mtaalamu Achiume amesema wakati dunia unaona ubaguzi huu lakini si suala jipya. “Ukweli ni kwamba wahamiaji na wakimbizi wasio wazungu wanakabiliwa na ubaguzi mbaya kote ulimwenguni wanapojaribu kuvuka mipaka ya kimataifa. Picha mbalimbali na ushuhuda kutoka kwa watu wasio wazungu wanaojaribu kutoroka Ukraine unathibitisha ukweli huu, na wanapaswa kuhamasisha hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa dhuluma ya kibaguzi na chuki dhidi ya wageni  iwe rasmi au hata isiyo rasmi inakomeshwa.”

Mtaalamu huyo amewasihi maafisa wa serikali, mashirika ya kibinadamu na wahusika wengine ikiwa ni pamoja na Muungano wa Ulaya na wanachama wake wachukue hatua za haraka ili kuhakikisha ulinzi wa watu binafsi na makundi yote yanayokabiliwa na ubaguzi wa rangi na kikabila wanapojaribu kukimbia Ukraine.

Mama akiwa na mtoto wake wake wa kiume wa miaka miwili baada ya kuondoka Odessa na kuingia nchini Romania  kupitia mpaka wa Isaccea
© UNICEF/Ioana Moldovan
Mama akiwa na mtoto wake wake wa kiume wa miaka miwili baada ya kuondoka Odessa na kuingia nchini Romania kupitia mpaka wa Isaccea

UNHCR

Kwingineko shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeeleza takwimu za watu waliokimbia Ukraine ni zaidi ya Milioni moja.

Watu hao wanaokimbia wanakimbilia nchi jirani za Poland, Hungary, Moldova, Slovakia, Romania na nchi nyingine za Muungano wa Ulaya. 

Kupata takwimu za kila dakika kadri watu wanavyokimbilia nchi jirani bofya hapa

UNESCO na ILO

Nayo mashirika ya UNESCO na ILO yameunga mkono azimio lililopitishwa tarehe 02 machi 2022 na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika mkutano wa dharura wa Baraza Kuu kujadili kuhusu mashambulizi yanayofanywa na Urusi nchini Ukraine.