KWA UFUPI: UKRAINE/COVID-19/VIUAVIJIUMBE MARADHI

Mtoto wa kike akiwasili Romania kusaka hifadhi kutokana na mapigano  yanayoendelea nchini Ukraine
© UNICEF/Ioana Moldovan
Mtoto wa kike akiwasili Romania kusaka hifadhi kutokana na mapigano yanayoendelea nchini Ukraine

KWA UFUPI: UKRAINE/COVID-19/VIUAVIJIUMBE MARADHI

Wahamiaji na Wakimbizi

Kama  kawaida ya siku ya Jumatano tuna muhtasari na leo umemulika:

-Jukwaa la kuonesha idadi ya wanaokimbia Ukraine kutokana na mashambulizi kutoka Urusi

-Changamoto ya wakimbizi kupata chanjo dhidi ya COVID-19

-Kuelekea Baraza Kuu la Mazingira, wito watolewa kuhakikisha viuavijiumbe maradhi havichafui mazingira

WAKIMBIZI UKRAINE

Idadi ya watu waliokimbia mashambulizi nchini Ukraine katika kipindi cha siku 6 zilizopita ni zaidi ya 870,000, limesema hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, kupitia jukwaa lake lililozindua ili kuonesha takwimu za watu wanaokimbia wakiwemo raia na wageni.
Jukwaa hilo lililoko mtandaoni linaonesha kuwa wakimbizi hao wameelekea nchi 8 za Ulaya  zikiwemo Poland, Hungary na Moldova. UNHCR inasema hivi wato hao wanahitaij ulinzi na misaada ya kibinadamu na kwamba hali inavyozidi kubadilika, watu wengine milioni 4 wanatarajiwa kukimbia Ukraine katika wiki au miezi ijayo.

COVID-19 NA WAKIMBIZI

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema ingawa nchi nyingi duniani zimejumuisha wakimbizi katika mipango yao ya utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19, bado wakimbizi wengi wanashindwa kupata chanjo hiyo kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo kukosa nyaraka za kujisajili kupata chanjo hiyo. Mkugenzi wa UNHCR anayehusika na masuala ya mnepo na majawabu Sajjad Maliki amesema hii leo kuwa ili kujisajili au ili kupata chanjo baadhi ya nchi zinahitaji nyaraka ambazo mara nyingi wakimbizi hawana. Nchi nyingine zimeanzisha mfumo wa kujisajili mtandaoni ambao unaweza kuzuia watu wasio na mtandao au wasio na uelewa wa kompyuta kushindwa kupata chanjo hizo. Kwingineko maeneo ya kupata chanjo yako mbali kutoka makazi ya wakimbizi au kuna masharti ambayo yanasababisha wakimbizi waripotiwe uhamiaji.

VIUAVIJIUMBE MARADHI VISICHAFUE MAZINGIRA

Na kundi ongozi la kimataifa katika kukabili usugu wa viuavijiumbe maradhi hii leo limetoa wito kwa nchi zote duniani kupunguza taka za viuavijiumbe maradhi zinazotupwa hovyo na kuharibu mazingira kwa kutaka kufanyika utafiti zaidi na kuchukua hatua za kutupa kwa uangalifu taka hizo za dawa kutoka kwenye vyakula na mifumo ya afya ya binadamu, Wanyama pamoja na viwandani. Wametoa wito huo kwenye mkutano wa Baraza la shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEA unaomalizika leo jijini Nairobi Kenya ambao umejadili changamoto kubwa za mazingira zinazokabili dunia. Mkutano huo ulianza tarehe 28 mwezi uliopita.