Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa imetosha vita vya Urusi nchini Ukraine lazima vikome sasa: Baraza Kuu

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akihutubia wajumbe wa Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu kuhusu Ukraine.
UN Photo/Evan Schneider
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Abdulla Shahid akihutubia wajumbe wa Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu kuhusu Ukraine.

Sasa imetosha vita vya Urusi nchini Ukraine lazima vikome sasa: Baraza Kuu

Amani na Usalama

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekutana leo kwa kikao maalum cha dharura kuhusu hali ya Ukraine.

Kikao hiki kinafanyika kufuatia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kupitisha azimio la kuiwajibisha Urusi kwa uvamizi wa Ukraine wiki iliyopita na hivyo mwishoni mwa wiki kupiga kura ya kuitisha kikao hiki cha dharura.  

Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Kuitishwa kwa mkutano huu maalum wa 11 wa dharura wa Baraza Kuu, unaotokana na katiba ya Umoja wa Mataifa kwa mujibu wa azimio namba 377 A lenye kichwa “Kuungana kwa ajili ya amani”, ni fursa mpya ya kuhakikisha kwamba uongozi wa Umoja wa Mataifa unazingatia kanuni za Umoja wa Mataifa na matarajio ya watu tunaowahudumia katika masuala yanayohusu amani na usalama.”  

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia wajumbe wa Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine.
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia wajumbe wa Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukraine.

Wakati wa kumaliza vita ni sasa 

Bwana Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja vita vinavyoendelea Ukraine. 

“Mapigano nchini Ukraine lazima yasitishwe. Yanavuma nchi nzima kuanzia angani, nchi kavu na baharini. Hili lazima likome sasa,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema katika mwanzo wa mkutano huo wa dharura. 

Ameongeza kuwa "Makombora ya Urusi na mashambulio ya angani yanapiga miji ya Ukraine mchana na usiku, kukithiri huku kwa vurugu zinakosababisha vifo vya raia wakiwemo watoto ni jambo lisilokubalika kabisa, imetosha, imetosha. Wanajeshi lazima warudi kwenye ngome zao. Viongozi lazima waelekezwe kwenye amani. Raia lazima walindwe”. 

Mkutano huu wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliandaliwa kwa ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wajumbe wa baraza, katika upigaji kura wa kiutaratibu siku ya Jumapili, walipitisha azimio la kutaka kikao hiki maalum kifanyike. 

Tangu mwaka 1950, Baraza la Usalama, ambalo lina wajumbe kumi na watano, ni mara chache sana limetumia utaratibu huu kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza Kuu, unaoleta pamoja nchi 193 wanachama. 

Siku ya Ijumaa, Urusi ilipinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama ambalo lilichukizwa na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.  

China, India na Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu au Emarati zilijizuia kupiga kura huku wanachama 11 waliosalia wakipiga kura ya ndio na Urusi kura ya hapana. 

Sasa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitapata fursa ya kuzungumza kwenye kikao hicho maalum ikiwa ni pamoja na makundi ya kanda mbalimbali kabla ya maamuzi ya mapendekezo ya Baraza hilo kuhusu nini kitakachofuata. 

Mara ya mwisho Baraza la Usalama kuomba kuitishwa kwa kikao maalum cha Baraza Kuu ni takriban miaka 40 iliyopita. 

Mnamo tarehe 26 Februari 2022 magharibi mwa Ukrainia, mama na mtoto waliokimbia makazi yao wanatembea kuelekea kituo cha ukaguzi cha Uzhhorod-Vyshne Nemetske ili kuvuka mpaka na kuingia Slovakia kutoka Oblast ya Zakarpattia.
© UNICEF/Yanosh Nemesh/UNIAN
Mnamo tarehe 26 Februari 2022 magharibi mwa Ukrainia, mama na mtoto waliokimbia makazi yao wanatembea kuelekea kituo cha ukaguzi cha Uzhhorod-Vyshne Nemetske ili kuvuka mpaka na kuingia Slovakia kutoka Oblast ya Zakarpattia.

Zahya ya Ukraine isiposhughulikiwa itakuwa zahama yetu sote

 

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu Abdulla Shahid, akifungua kikao hicho, amesema chombo hicho, pamoja na nchi wanachama  wake 193, "kinawakilisha dhamira ya pamoja ya ubinadamu."

 

Ameongeza kuwa "Nguvu ya Baraza hili inatokana na mamlaka yake ya kimaadili. Tudhihirishe ujasiri huo wa kimaadili na tuutumie mjadala wa leo sio kupiga porojo za vita, bali kuipa amani nafasi. Tuwashe moto wa upendo, utu na huruma. . Bunduki ni bora zaidi zikifungwa na kusalia kibindoni. Acha amani itawale."
Ameendelea kusema kuwa hatua ya leo ya wawakilishi kutoka Ukraine na Urusi kukutana kuzungumza nchini Belarus ni dalili Njema akitumai kwamba huenda ikasaidia kumaliza jinamizi hili la vita na kufungua tena mlango wa matumaini ya majadiliano ya amani.