Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola milioni 20 kusaidia mahitaji ya dharura ya kibinadamu Ukraine

Shule iliyotelekezwa, iliyoharibiwa baada ya kupigwa na makombora, huko Krasnohorivka, Mkoa wa Donetsk, Ukraine. (faili)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Shule iliyotelekezwa, iliyoharibiwa baada ya kupigwa na makombora, huko Krasnohorivka, Mkoa wa Donetsk, Ukraine. (faili)

CERF yatoa dola milioni 20 kusaidia mahitaji ya dharura ya kibinadamu Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa  umetenga dola za Marekani milioni 20 kutoka mfuko wake wa misaada ya dharura (CERF) ili kusongesha mara moja msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha na ulinzi kwa raia nchini Ukraine kufuatia ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi. 

Fedha hizo zitasaidia operesheni za dharura za kibinadamu kwenye za dharura kwenye eneo la makabiliano katika majimbo ya Mashariki ya Donetska na Luhanska na katika maeneo mengine ya nchi. 

Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakuratibu masuala ya kibinadamu Martin Griffiths ameonya kwamba ongezeko la operesheni za kijeshi litakuwa na athari kubwa kwa maisha ya raia, na akasisitiza wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitishwa kwa mapigano mara moja. 

"Fedha za CERF zinaokoa maisha. Zitasaidia kwa huduma za afya, malazi, chakula, maji na usafi wa mazingira kwa watu walio hatarini zaidi ambao wameathiriwa na vita, wakiwemo wanawake, watoto na wasichana, wazee na waliokimbia makazi yao." amesema Bwana. Griffiths.  

Fedha zitakavyotumika 

Kwa mujibu wa shirika la kuratibu misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA  “Fedha hizo pia zitasaidia kuzuia unyanyasaji wa kijinsia na huduma zingine zinazohusiana na ulinzi, pamoja na elimu, vifaa na mawasiliano ya simu.” 

Kabla ya kuongezeka kwa machafuko ya hivi karibuni , OCHA inasema watoto wapatao milioni 2.9, wanawake na wanaume tayari walikuwa wameathiriwa na miaka minane ya mzozo mashariki mwa Ukraine, na washirika wa kibinadamu walihitaji dola milioni 190 kusaidia watu milioni 1.8 walio hatarini zaidi nchini humo. 

Bwana Griffiths amesisitiza kuwa “Tunahitaji haraka kuongezwa fedha za ufadhili wa misaada ya kibinadamu, kwani kutakuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji msaada.” 

Ameongeza kuwa shughuli za kibinadamu nchini Ukraine na kwingineko zinaongozwa na kanuni zinazotambulika kimataifa za ubinadamu, kutoegemea upande wowote, kutopendelea na uhuru wa kiutendaji. 

CERF ni mojawapo ya njia za haraka na bora zaidi za kuhakikisha kuwa usaidizi unaohitajika haraka unawafikia watu walio katika matatizo.  

CERF iliyoanzishwa kama hazina ya wafadhili, huwezesha watoa huduma za kibinadamu kutoa usaidizi wa kuokoa maisha wakati wowote na popote pale ambapo majanga yanatokea.