Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Wakimbizi kutoka ukraine wakisubiri basi ili waendelee na safari yao baada ya kuvuka mpaka wa Poland

Hakuna njia nyingine bali ni kuwahamisha watu Mariupol Ukraine: WFP/ICRC

© UNICEF/Tom Remp
Wakimbizi kutoka ukraine wakisubiri basi ili waendelee na safari yao baada ya kuvuka mpaka wa Poland

Hakuna njia nyingine bali ni kuwahamisha watu Mariupol Ukraine: WFP/ICRC

Msaada wa Kibinadamu

Juhudi za kuwasaidia maelfu ya wakaazi waliokata tamaa kukimbia mji uliokumbwa na mapigano makali nchini Ukraine wa Mariupol zimeendelea leo Ijumaa, huku wasaidizi wa kibinadamu wakionya kwamba hakuna njia nyingine kwa watu hao isipokuwa kuondoka baada ya wiki za mashambulizi ya mara kwa mara tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi tarehe 24 Februari. 

Mchakato huo unafuatia jaribio la awali la kuwahamisha raia kutoka mji huo wa bandari wa kusini mwanzoni mwa Machi, hadi kuanza tena kwa mapigano kulipokatiza matumaini ya kutoka kwa usalama kwa wale wanaotaka kuondoka. 

Familia zafika Berdyszcze nchini Poland, baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine, wakikimbia mzozo unaozidi kuongezeka.
© UNICEF/Tom Remp
Familia zafika Berdyszcze nchini Poland, baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine, wakikimbia mzozo unaozidi kuongezeka.

Hali ya sintofahamu miongoni mwa wakazi  

“Tunabakia kuwa na matumaini, tuko katika hatua, tukielekea Mariupol, hilo ni jambo zuri; lakini bado haijabainika kuwa hili litafanyika leo,” amesema Ewan Watson, msemaji wa Kamati ya Kimataifa ya chama cha Msalaba Mwekundu (ICRC) akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo.

Ameongeza kuwa "Iwapo itafanyika na lini, jukumu la ICRC kama mpatanishi wa pande zote litakuwa kuongoza msafara kutoka Mariupol hadi mji mwingine nchini Ukraine. Hatuwezi kuthibitisha ni jiji gani kwa sasa kwani hili ni jambo ambalo wahusika lazima wakubaliane nalo.” 

Msafara uko tayari 

Zaidi ya mabasi 50 yanatarajiwa kutoka Mariupol, yakisindikizwa na magari mengine ya kiraia na ya ICRC, kutoa kuonyesha ishara ya kibinadamu kwenye kwenye safari hizo na kutoa ulinzi wa ziada kwa msafara, ameongeza msemaji wa ICRC  

Amesisitiza kuwa "Hakuna mpango mwingine hapa, tumekuwa tukifanya kazi kwa wiki na kuwaambia vyombo vya habari juu ya juhudi zetu za kuingia Mariupol kwa msaada na kuruhusu njia salama ya raia kutoka nje ya jiji. Kwanu muda unayoyoma kwa watu wa Mariupol.” 

Kote nchini Ukraine, mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuwa mbaya na kuongezeka kwa kasi limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa Chakula WFP

Shirika hilo limewasilisha msaada wa chakula cha kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na chakula kilichopikwa tayari kuliwa, mikate na msaada wa pesa taslimu, kwa watu milioni moja walioathiriwa na vita. "Watu wana msongo wa mawazo na hawana chaguo," amesema msemaji wa WFP Tomson Phiri. "Mpango wetu  ni kusaidia watu zaidi na zaidi, tunataka kufikia angalau watu milioni tatu katika wiki na miezi ijayo", ameongeza. 
WFP tayari imetoa takriban tani 40,000 za chakula, unga wa ngano na mgao wa chakula nchini Ukraine na nchi jirani kwa ajili ya usambazaji. 

Nje ya Ukraine, shirika hilo linapanga kusaidia wakimbizi 300,000 na watu wanaotafuta hifadhi ambao wamepata hifadhi katika nchi jirani, miongoni mwa watu milioni 4.1 ambao wamekimbia mapigano, kulingana na takwimu za hivi karibuni za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR

Wafanyakazi wa misaada wanatayarisha usaidizi unaohitajika sana kutoka kwa msafara wa mashirika ya kibinadamu unaoongozwa na Umoja wa Mataifa uliofika Sumy, Ukraine.
© UNOCHA/Laurent Dufour
Wafanyakazi wa misaada wanatayarisha usaidizi unaohitajika sana kutoka kwa msafara wa mashirika ya kibinadamu unaoongozwa na Umoja wa Mataifa uliofika Sumy, Ukraine.

Msaada kwa Kharkiv na Sumy 

Bwana Phiri amesema licha ya kuendelea kwa ghasia ambazo zimejumuisha makombora na mapigano mitaani, "WFP imepeleka chakula kwa familia zilizo hatarini katika miji iliyozingirwa ya Kharkiv na Sumy, kupitia misafara miwili ya misaada ya kibinadamu ambayo imefika katika maeneo yenye migogoro". 

Ameongeza kuwa "Moja ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo hapa ni kwamba hakuna washirika wengi wa kibinadamu ambao wanaweza kufanya kazi katika maeneo yaliyozingirwa." 

Mjini Kharkiv, WFP pia imesambaza mikate 330,000 mipya iliyookwa na inapanua wigo wa mpango huu wa kutengeneza mikate katika miji mingine, kwa lengo la kuwasilisha watu mikate mingine 990,000 katika wiki zijazo. 

WFP pia imewasilisha akiba ya vifurushi vya chakula vya msaada wa haraka huko Dnipro na Kirovohrad katikati mwa Ukraine, na Vinnytsia katika eneo la kati-magharibi, kwa kutumia misafara ya mashirika wadau kwa ajili ya kutumiwa na washirika wa WFP. 

Phiti ameongeza kuwa katika maeneo ambayo yameathiriwa na vita lakini sio kwa njia ya moja kwa moja  na ambapo chakula kinapatikana na maduka ya reja reja yanafanya kazi kama kawaida, WFP imeanza kutoa pesa taslimu au vocha kama njia ya msaada.