Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaahidi msaada zaidi kwa wakimbizi wa ndani Ituri, DRC

Watu waliokimbia makazi yao wakati wa kuwasili kwa Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani huko Roe, DRC.
© UN Photo/Eskinder Debebe
Watu waliokimbia makazi yao wakati wa kuwasili kwa Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani huko Roe, DRC.

UN yaahidi msaada zaidi kwa wakimbizi wa ndani Ituri, DRC

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema utashirikiana na mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, pamoja na wadau wake wengine ili kuhakikisha kuna usalama mashariki mwa Taifa hilo, amesema Jean-Pierre Lacroix Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa. 

Alikuwa akizungumza Goma,mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, wakati wa siku yake ya kwanza ya ziara yake nchini humo akimwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa Antonoi Guterres. 

Bwana Lacroix alikuwa na mazungumzo kwa nyakati tofauti na viongozi wa majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ambako amesisitiza umuhimu wa jamii ya kimataifa kusaidia DRC katika kulinda wananchi wake ikwemo jimboni Ituri ambako mashabulizi ya mara kwa mara kutoka wanamgambo wa CODECO kwenye mji wa Djugu yamesababisha vifo vya mamia ya watu huku maelfu wakisalia wakimbizi wa ndani. 

Usalama wa ndani ni kipaumbele 

Bwana Lacroix ametembelea eneo la Umoja wa Mataifa huko Djugu jimboni Ituri ambako ni makazi ya mmuda kwa watu 74,000 na kuzungumza na wawakilishi wa jamii zinazoshi kwenye eneo hilo. 

Wawakilishi hao wamekuwa na maombi tofauti kwa Umoja wa Mataifa na pia kwa serikali kwa kuzingatia kuwa Waziri wa Ulinzi wa DRC Gilbert Kabanda alikuwa ameambatana na Bwana Lacroix wakati wa mazungumzo hayo. 

Waziri Kabanda aliahidi kuwa ndani ya mwezi mmoja, ulinzi utakuwa umeimarishwa kwenye vijiji ambako wananchi walikkimbia ili ulinzi uweze kuwa kamilifu na miundombinu kama vile shule na vituo vya afya viweze kujengwa. 

Mmoja wawakilishi wa jamii hizo ni Pilo Mulindro Willy ambaye ni Chifu wa Bulkwa ambaye aliibua suala la usalama kupatiwa kipaumbele kote katika eneo hilo la makazi ya muda pamoja na kule walikokimbia wakimbizi hao. 

“Naiomba serikali ipokonye silaha haya makundi yaliyojihami kwa kuwa wanasumbua watu. Wanavijiji wanataka kurejea nyumbani ili waendelee na kilimo,” amesisitiza. 

“Tunataka serikali itume askari wengi zaidi kulinda vijiji vyetu,” alisema na kuongeza kuwa ahadi ya mwezi mmoja ni ndefu mno kusubiri kwa askari kupelekwa na ulinzi kuimairishwa. 

Waziri Kabanda alitambua kuwa eneo la Roe si salaha kwa kuwa hakuna askari wa kutosha kutoka jeshi la DRC kuweza kulinda raia. 

Mwananchi mkimbizi wa ndani aliwa amebeba kuni huko Roe, DRC
© UN Photo/Eskinder Debebe
Mwananchi mkimbizi wa ndani aliwa amebeba kuni huko Roe, DRC

Wanawake wanataka ulinzi mahsusi 

Miongoni mwa wanawake wawakilishi ambao Bwana Lacroi alikutana nao ni Beatrice Manyotsi ambaye aliieleza Idhaa ya Umoja wa Mataifa baada ya mazungumzo hayo kuwa wanahitaji suluhu ya kudumum ya matatizo ya ukosefu wa usalama. 

“Tunashukuru mazungumzo na Umoja wa MAtaifa hii leo kwa kuwa ni muda mrefu hatujapata fursa kama hii. Tunashukuru mno kwa sababu mikutano kama hii inaweza kutupatia suluhisho la kudumu kwa matatizo yanayokumba DRC na hususan Ituri,” alisema Bi. Manyotsi. 

Alifunguka zaidi kuhusu changamoto mahsusi zinazokumba wanawake ikiwemo ghasia na mauaji. “Wanawake wa DRC wanaishi maisha magumu, wanawake wanauawa, wanawake wanakatwa viungo, tuko kama kifaa kisicho na thamani yoyote. Hakuna elimu kwa watoto wetu. Tunataka Umoja wetu wa Mataifa utusaidie sisi kwa sababu watoto wa DRC ndio watoto wa kesho. Iwapo wanaishi mazingira duni kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, mathalani, basi mustakabali wao utakuwa mashakani.” 

Bi. Manyotsi ameunga mkono wito wa Chifu wa Bulkwa kwamba usalama lazima upatiwe kipaumbele. “Hatuwezi kwenda kuteka maji, kuchanja kuni wala kulima kwa sababu tunapata vitisho kutoka makundi yaliyojihami.” 

Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa MAtaifa, wimbi la mashambulizi ya kutumia silaha huko Ituri tangu mwezi Novemba mwaka jana wa 2021 yamesababisha ongezeko la wakimbizi wa ndani huko Roe na hivyo mahitaji ya huduma kuongezeka haraka. 

Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani akiwasili Bunia, DRC
© UN Photo/Eskinder Debebe
Naibu Katibu Mkuu wa Operesheni za Amani akiwasili Bunia, DRC

Mahitaji ya kibinadamu yameongezeka 

Kwa sasa hali ya miundombinu na huduma za msingi kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani hakuna, na hivyo wengine wanakimbilia maeneo ya umma huku wengine wakisaka hifadhi kwa wenyeji. 

Kwa sasa, wakimbizi wa ndani hawana huduma ya malazi, maji, afya na usaidizi wa kisaikolojia. 

Wakimbizi wapya wa ndani hawana huduma za msingi na vifaa muhimu na hivyo kuongeza shinikizo zaidi kwa wakimbizi waliokuweko kambini miezi sita iliyopita. 

Huduma za kujisafi na usafi ni muhimu kutokana na hatari inayowezekana ya kuwepo kwa magonjwa hatari ya mlipuko kwa kuwa hakuna huduma za maji safi na kujisafi.  

Tunashikana na wananchi wa DRC 

Baada ya safari ya dakika 15 kwa helikopta kutoka Roe hadi Bunia, Ituri, Bwana Lacroix alisafiri hadi Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu KAskazini, ambako alikuwa na mazungumzo na gavana wa kijeshi wa Goma, Luteni Jenerali Ndima Constant. 

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa akasisitiza mshikamano na wananchi wa DRC. 

“Katibu Mkuu anatuma ujumbe wake kuhusu azma yetu ya kufanya kazi bila kuchoka kwa ushirikiana na mamlaka za jeshi, kitaifa na kijimbo pamoja na mashirika ya kiraia nawatoa huduma za kibinadamu sambamba na azma yetu ya kuona wananchi wananufaika na ombi letu la kibinadamu na juhudi za kijeshi za ulinzi,” amesema Bwana Lacroix akiongeza kuwa ziara yake imedhihirisha uhusiano wa dhati ulioko kati ya Umoja wa Mataifa na mamlaka za jimbo. 

Kuhusu ulinzi wa raia mjini Goma, Bwana Lacroix ametaja ushirikiano aliosema ni mkubwa ulioanzishwa kati ya jeshi la serikali ya DRC, FARDC na moja ya nchi jirani na DRC. 

“Nadhani azma ya aina hii inazaa matunda, lakini sote tunaelewa inachukua muda na ndio maana sisi Umoja wa MAtaifa tumekuwa tukirudia ujumbe mara kwa mara wa maombi yetu na ushiriki wa mazungumzo. Unaweza kuwa umeazimia lakini wakati huo huo unaelewa kuwa si tatizo la kumalizika katika kipindi cha wiki au miezi,” Amesema. 

Tarehe 17 mwezi huu wa Februari, serikali ya DRC na wadau wa kibinadamu walizindua ombi la dola Bilioni 1.88 kutekeleza ombi la kibinadamu ya taifa hilo kw a mwaka 2022 zikilinga watu milioni 8.8 walio hatarini zaidi. 

Alhamisi, Bwana Lacroix atakuwa mji mkuu wa DRC, Kinshasa ambako atashiriki mkutano wa 10 wa mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa makubaliano na amani, usalama na ushirikiano maziwa makuu, ROM uliotiwa saini mwaka 2013 huko Addis Ababe Ethiopia.