Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa UN waonya juu kuongezeka kwa ghasia Sudan Kusini

Watoto wakichungulia nje kupitia dirishani nchini Sudan Kusini.
© UNMISS/Amanda Voisard
Watoto wakichungulia nje kupitia dirishani nchini Sudan Kusini.

Wataalamu wa Haki za Binadamu wa UN waonya juu kuongezeka kwa ghasia Sudan Kusini

Wahamiaji na Wakimbizi

Wajumbe wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Kusini wamekamilisha ziara yao ya tisa iliyodumu kwa wiki moja ambapo wamezuru katika maeneo ya Juba na Yei.

Wakiwa huko wajumbe wa tume hiyo wakekuwa na majadiliano na watu mbalimbali na taasisi, ili kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini ambapo Mwenyekiti wa Tume hiyo Yasmin Sooka amesema, “kuna makubaliano kati ya washikadau wakuu kwamba ingawa baadhi ya mafanikio yamepatikana katika kutekeleza Mkataba Uliohuishwa, vipengele muhimu vinavyohusisha mageuzi ya sekta ya usalama, mageuzi ya kikatiba na uchaguzi, na haki ya mpito bado hayajashughulikiwa. Masuala haya yote ambayo hayajakamilika yanaathiri hali ya haki za binadamu nchini humu.”

Sooka ameongeza kuwa, “Wasudan Kusini wengi ambao Tume ilizungumza nao walionesha nia yao ya uongozi wa kisiasa kupata amani na haki, ambayo Mkataba huo unatoa muongozo wa nini chakufanya.”

Kikao na Serikali

Makamishna hao walikutana na mawaziri wakuu wa Serikali na viongozi, wanachama wa asasi za kiraia, watu walionusurika katika ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, viongozi wa dini, vyombo vinavyofuatilia Mkataba wa Amani Uliohuishwa wa 2018, wanachama wa jumuiya ya wanadiplomasia ikiwa ni pamoja na kutoka Troika na Umoja wa Afrika, na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS).

Katika kikao cha Tume hiyo na Wizara ya Sheria, Tume ilithibitisha tena utayari wake wa kuunga mkono Serikali kutekeleza kikamilifu Sura ya Tano ya Makubaliano ya Amani, kwa kuzingatia mapendekezo ya warsha ya pamoja ya Tume iliyoitisha Nairobi, Kenya, Desemba 2021.

Malalamiko ya wadau

Wanachama wa mashirika ya kiraia ya Sudan Kusini waliokutana na Tume hiyo walisema wanaogopa kujadili hali ya haki za binadamu, kwa kuhofia kulipiziwa kisasi na vyombo vya usalama vya Serikali vilivyo na rekodi ya kukandamiza maoni makali ya kisiasa.

“Sudan Kusini iko pembezoni kabisa. Ufuatiliaji wa uchaguzi una hatari kubwa ya kuchochea ghasia na mgawanyiko ikiwa taasisi zinazohitajika, sheria za kikatiba na uchaguzi pamoja na mipangilio ya vifaa hazitawekwa kwanza.” Akasisitiza Kamishna Barney Afako.

Kamishna huyo pia amesema ni muhimu kuangalia zaidi ya wakati wa uchaguzi na kuuliza ni mfumo gani wa kisiasa ambao watu wangepigia kura, hasa kutokana na kucheleweshwa kwa kuunda katiba ambayo uchaguzi ungetegemea.

Wajumbe hao wamesema kazi moja kuu itakuwa kuainisha maeneo ya majimbo ya ubunge ya uchaguzi.

Swali kubwa zaidi linajitokeza kuhusiana na mfumo ambao watu watakuwa wakiupigia kura, kutokana na kukosekana kwa katiba ya kudumu, na ukosefu wa ufafanuzi wa sasa wa jinsi mfuatano wa chaguzi na utungaji katiba unavyopaswa kuingiliana.