Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wito wazinduliwa kuchagiza uchangishaji wa fedha kwa ajili ya jukwaa la kutokomeza COVID-10

Mwanamke akipewa chanjo ya COVID-19 huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Jospin Benekire
Mwanamke akipewa chanjo ya COVID-19 huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wito wazinduliwa kuchagiza uchangishaji wa fedha kwa ajili ya jukwaa la kutokomeza COVID-10

Afya

Hii leo viongozi wa dunia akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wamezindua wito kutokomeza janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 mwaka huu wa 2022 kama dharura ya kimataifa kwa kuchagiza uchangiaji wa wa fedha kwenye jukwaa la vifaa vya kutibu Corona, ACT. 

Jukwaa hilo ni ubia wa mashirika yanayoongoza kwa kupatia nchi za kipato cha chini na kati vifaa vya uchunguzi wa COVID-19, matibabu, chanjo na vile vya kujikinga.

Akihutubia mkutano huo kwa njia ya video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema usawa katika utoaji wa chanjo lazima uanzie katika mfumo mzima wa usambazaji wa chanjo hizo.  

“Tunaingia mwaka wa tatu wa janga hili, na dunia bado iko mbali kabisa kufikia malengo muhimu. Kuchanja watu wote, kuongeza upimaji, kuhakikisha matibabu muhimu yanafikia kila mtu. Halikadhalika wahudumu wa afya walio mstari wa mbele wa vifaa bora vya kujikinga,” amesema Guterres. 

Ukosefu wa uwiano wa kukabili COVID-19 ni changamoto 

Amekumbusha kuwa ukosefu wa uwiano wa mgao wa chanjo ni kosa kubwa la kimaadili kwa zama za sasa na watu wengi wanagharimika. 

Hata hivyo amesema “habari njema ni kwamba maendeleo ya hivi karibuni yameonesha tunaweza kutoa huduma pindi tunapokuwa na rasilimali na kushirikiana. Usambazaji wa chanjo unakwenda kwa  kasi kubwa na tunafidia muda tuliopoteza. Tunakaribia kutokomeza janga hili, mwaka huu.” 

Guterres amesema ni lazima kukumbuka kuwa janga la Corona litaendelea kuwepo iwapo “hatutahakikisha vifaa vyote vinapatikana kwa kila mtu. Tuna mifumo ya kuchagiza usambazaji wa vifaa hivi muhimu,” amesema Katibu akitaja mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya WHO na la kuhudumia watoto, UNICEF ambayo kwa miongo kadha yamekuwa mstari wa mbele kusaidia nchi kuendesha kampeni za chanjo kwa ufanisi mkubwa. 

Mhudumu wa afya anajiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 katika kituo cha chanjo huko Luanda, Angola.
© WHO/Booming/Carlos Cesar
Mhudumu wa afya anajiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 katika kituo cha chanjo huko Luanda, Angola.

ACT ndio jawabu mujarabu 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu amesema “ACT inatoa njia ya kutoka katika janga la COVID-19, njia  iliyogharimiwa, iliyoratibiwa nah alali kwa kila mtu na kila pahali. Njia inafaa kufadhiliwa kwa uwiano wa michango kutoka nchi zote.” 

Katibu Mkuu amesema zaidi ya yote “tunahitaji uwekezaji wa wakati sahihi wa kusambaza chanjo na wakati huo upimaji. Hili ndio suala la usawa, ni suala la haki na ni suala la fikra kuzaliwa nayo ambayo zamani ilikuwepo.” 

Guterres amesema inawezekana kutokomeza janga hili mwaka huu. “Tunayo njia ya kufika hapo. Lakini tunaweza kufika hapo kwa pamoja. Ni juu yetu sisi na hii yote ni kwenye suala la usawa.” 

ACT ilizinduliwa mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2020 katika tukio lililokuwa limeandaliwa kwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Rais wa Ufaransa, Rais wa Kamisheni ya Ulaya na taasisi ya Bill na Melinda Gates.