Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume ya Haki ya Binadamu yaanza ziara nchini Sudan Kusini 

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, Sudan Kusini, kutoka kushoto Mwenyekiti Yasmin Sooka, Andrew Clapham na Barney Afako (2018).
UN Commission on Human Rights in South Sudan / Twitter screen grab
Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, Sudan Kusini, kutoka kushoto Mwenyekiti Yasmin Sooka, Andrew Clapham na Barney Afako (2018).

Tume ya Haki ya Binadamu yaanza ziara nchini Sudan Kusini 

Haki za binadamu

Wajumbe wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Kusini hii leo wanaanza ziara ya tisa nchini humo.

Ziara hiyo ya wiki moja inaongozwa na mwenyekiti wa tume hiyo Bi.Yasmini Sooka kutoka nchini Afrika Kusini na Barney Afako kutoka Uganda pamoja na makamishna wengine wawili, ambapo wanatarajiwa kukutana na mawaziri wa nchi hiyo, wanachama wa asasi za kiraia, viongozi wa dini , wanadiplomasia, vyombo vinavyofuatilia Mkataba wa Amani wa mwaka 2018, mashirika ya Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS).

Miongoni mwa shughuli wanazotarajiwa kufanya ni mikutano ya kujadili hatua na kuunga mkono zinazohitajika ili kutekeleza taratibu, haki za mpito, kama ilivyokubaliwa kwenye mkutano ulioandaliwa na kamisheni mwezi Desemba  2021 huko Nairobi, Kenya.

Wajumbe wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu watawasilisha ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi 2022, mjini Geneva Uswisi.

Kuhusu Tume

Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Sudan Kusini ni chombo huru kilichoanzishwa mwaka 2016 na kupewa mamlaka na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.

Tume hiyo ina jukumu la kuchunguza hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini, na kuamua na kuripoti ukweli na hali ya ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukwaji, ikiwa ni pamoja na kufafanua wajibu wawahusika wa ukiukwaji huo ambao ni uhalifu chini ya sheria za kitaifa na au za kimataifa.

Ili kusaidia katika uchunguzi rasmi wa kisheria nchini Sudan Kusini, Tume pia ina jukumu la kukusanya na kuhifadhi ushahidi, na kuhakikisha ushahidi huo unapatikana  pale mifumo ya haki inapohitaji, ikiwa ni pamoja na mahakama ya mseto ya Sudan Kusini ambayo itaundwa chini ya Sura ya 5 ya Mkataba wa Amani Uliohuishwa. ya 2018.