UNMISS yatoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana wa Sudan Kusini

27 Aprili 2021

Nchini Sudan Kusini, kwenye mji wa Aweil, vijana 40 wa kiume na wa kike wamesema wananufaika na mafunzo ya ufundi kwa miezi mitatu yanayotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Katika kituo cha mafunzo ya ufundi, mjini Aweil, wanawake wanaonekana wakijifunza kuoka mikate, wanaume wakijifunza useremala. Josephine Anger, mmoja wa wanawake wanaopata mafunzo, anasema alikuwa na shauku kuhusu maisha yake ya baadaye na yote aliyojifunza wakati wa mwezi wake wa kwanza kuhudhuria mafunzo haya ya ufundi. “Kituo hiki cha ufundi ni kweli kimenisaidia sana. Kimefungua macho yangu, akili yangu na moyo wangu. Kwa kufanya kozi hii ya kuoka mikate, ni kama  naona picha kadhaa za kutengeneza mkate, keki, aina tofauti za pipi na chakula kingine. Hapo awali, hata sikujua jinsi ya kutengeneza mkate, lakini sasa ninaenda sokoni kununua unga na kuiandaa nyumbani kwa familia yangu. Kabla nilikuwa nalazimika kununua kutoka sokoni hata wakati sikuwa na pesa. " 

Thomas Mtaisi, ni kiongozi wa timu ya Usaidizi, Utengamano na Ulinzi kutoka UNMISS anasema,  "Yote haya yatasaidia katika useremala, uokaji na ujuzi wa usimamizi wa biashara. Zaidi ya hapo, mwisho wa mradi walengwa wataenda nyumbani na kifurushi, kifurushi cha kuanzia ambacho kitawasaidia kuanza biashara zao na kuendelea.” 

Bwana Mtais pia anaeleza kuwa kwa kuwaandaa vijana kwa ajili ya soko la ajira, mradi huu wa mafunzo ya ufundi hatimaye unakusudia kuzuia mizozo inayosababishwa na ukosefu wa rasilimali, kukosa la kufanya, au vyote viwili,   "Tuna nia ya kusaidia vijana kwa sababu, kimsingi, jimbo la Kaskazini mwa Bahr El Ghazal, kumekuwa na amani kwa kiasi fulani. Tulihisi kuwa vijana wanapaswa kupata gawio la amani na hii inaweza pia kuwa shughuli ya majaribio ambayo inaweza kufanyika katika majimbo mengine.” 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter