Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS waendesha warsha kwa wanawake ya kutoa mafunzo ya kutatua mizozo

Wanawake wakizungumza kwenye kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Sudan Kusini. Kushoto ni Dudu Emilia.
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Wanawake wakizungumza kwenye kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Sudan Kusini. Kushoto ni Dudu Emilia.

UNMISS waendesha warsha kwa wanawake ya kutoa mafunzo ya kutatua mizozo

Haki za binadamu

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la kupinga ukatili kwa ajili ya amani wameaanda warsha ya wawakilishi wanawake takriban themanini kuhusu namna ya kuzuia mizozo na kulinda haki za binadamu.

Katika kambi ya Rimenza inayozingira kanisa la Equatoria magharibi nchini Sudan Kusini shughuli za kila siku zinaendelea lakini kwa upande mwingine, washiriki wa warsha wanabadilishana uzoefu wao kuhusu mbinu za kutatua mizozo kwa lengo la kuwa mabalozi wa amani katika jamii yao.

Washiriki wanafanya zoezi kwa vitendo ni katika kuelimishwa kuhusu kutatua mizozo kwa njia ya amani 

Mmoja wa washiriki ni Mama Tubi Festus mkazi wa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Rimenze,“Tumejifunza mengi kuhusu mizozo, jinsi ya kukabiliana nayo na ni nini athari zitokanazo na mzozo ambao zinaathiri jamii yetu.”

Washiriki hao wamepata wataalamu ambao wamewaelimisha kuhusu mizozo na hivyo wana matumaini katika kukabiliana na hilo kama anavyoafiki Mary Papai Wangu, mkazi wa kambi ya Rimenze,“Kile ambacho nitafanya baada ya mafunzo haya ni kwamba, watu ambao nitakutana nao wanaokabiliwa na mzozo, nitajaribu kusuluhisha kwa kutumia stadi ambazo nimezipata katika warsha hii ya siku mbili.”

UNMISS inaamini kwamba ni muhimu kuimarisha wanawake kwa ajili ya kuhimiza uwiano katika jamii kama anavyosema Jackson Kambale, afisa wa maswala ya umma wa mpango huo

“Tuliwaza na kukubaliana na wanawake katika eneo hili kwamba wanahitaji stadi muhimu na mbinu za kuwasaidia kuchangia katika utengamano katika eneo hili na kujenga mahusiano thabiti miongoni mwao kwa ajili ya kukabiliana na mizozo ambayo huenda ikaibuka hapa.”

Na baada ya kukamilisha warsha, nyimbo na vigelegele vikatamalaki.

(Nats)