Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante UNMISS kwa kukarabati barabara kati ya Yambio na Mundri – Wananchi Sudan Kusini 

Kamanda wa kikosi cha UNMISS akizuru baadhi ya barabara zinazokarabatiwa nchini Sudan Kusini.
UN/Gregório Cunha
Kamanda wa kikosi cha UNMISS akizuru baadhi ya barabara zinazokarabatiwa nchini Sudan Kusini.

Asante UNMISS kwa kukarabati barabara kati ya Yambio na Mundri – Wananchi Sudan Kusini 

Amani na Usalama

Wananchi wa Sudan Kusini wanaoishi katika maeneo ya Yambio na Mundri wameshukuru Umoja wa Mataifa kwa ukarabati wa barabara katika maeneo ya Jimbo la Equatoria Magharibi ambayo yamekuwa hayafikiki wakati wa msimu wa mvua, lakini Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, kupitia kikosi chake cha uhandisi cha Bangladeshi sasa wanayarekebisha.

Miundombinu mibovu ya barabara ni mojawapo ya changamoto wanazokumbana nazo walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanapokuwa wakifanya doria nchini Sudani Kusini, hasa wakati wa msimu wa mvua. Kwa kawaida, inachukua takribani siku mbili kukamilisha umbali wa kilomita 230 kutoka Yambio hadi Mundri. Christopher Murenga, ni Mkuu wa Ofisi ya UNMISS iliyoko Yambio anasema, "Wakati barabara inapokuwa katika hali mbaya  kama ilivyokuwa kwa sehemu kubwa ya mwaka jana, ilikuwa inachukua miezi miwili hadi mitatu kupata vifaa. Kulikuwa na kipindi ambacho malori zaidi ya mia moja yalikwama kwenye barabara hiyo, bei za bidhaa huko Yambio zikapanda sana na maisha ya watu yalikuwa katika hali mbaya sana. Kwa hivyo, uboreshaji wa barabara utaboresha upatikanaji wa jamii na kufanya maisha kuwa bora. " 

Maendeleo ya ukarabati yaliyofikiwa hadi sasa tayari yanawanufaisha maelfu ya watu. Richard Enoka ni mwananchi wa Sudan Kusini, na sasa ana uwezo wa kutumia pikipiki yake tofauti na awali, anasema,  “Asante sana kwa UNMISS, sasa nina uwezo wa kuendesha pikipiki yangu kati ya Mambe na Maridi kwa saa moja na nusu badala ya saa tatu au hata nne. Ilikuwa mvua ikinyesha barabara inakuwa na matope na mambo mengi yanatokea katika barabara hiyo.” 

UNMISS pia, katika njia hiyo hiyo wanajenga daraja ambalo linaunganisha Maridi na vijiji ambavyo vina mchango muhimu katika kilimo.  

Wanajamii wa eneo hilo wanashukuru, kwani mazao yataweza kufikia soko na wakazi wataweza kupata huduma za msingi. Na hivyo wanashiriki katika shughuli hii, wanawake kwa wanaume wanachimba mitaro na wengine katika ufungaji wa nondo za daraja. Agness Leila ni mkazi wa eneo la Kuwanga ana hamu ya kuona daraja likikmilika, “Mkondo huu umekuwa shida kwa muda mrefu. Wakati umejaa hatuwezi kuuvuka, mazao yetu hayawezi kusafirishwa, na watoto wetu hawawezi kwenda shule. Tumepoteza watoto wengine kwenye mkondo huu wa maji. " 

Barabara iliyoboreshwa na daraja jipya vitakuwa na faida kubwa kwa maeneo kadhaa muhimu katika eneo hili la maridi. Kazi ya barabara ilianza mwezi Januari na inatarajiwa kufika Yambio mwezi ujao wa Mei.