Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nasimama katika mshikamano na watu wa Myamnar : Guterres

Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.
UNOCHA/Z. Nurmukhambetova
Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.

Nasimama katika mshikamano na watu wa Myamnar : Guterres

Amani na Usalama

Ikiwa hapo kesho Jumanne, Februari 1,2022 ni maadhimisho ya mwaka mmoja tangu jeshi la Myanmar kupindua Serikali ya kiraia iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na kuwaweka kizuizini kiholela viongozi wa Serikali, akiwemo Mshauri wa Serikali Aung San Suu Kyi na Rais Win Myint. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anasimama katika mshikamano na watu wa Myanmar na matarajio yao ya kidemokrasia kwa jamii jumuishi na ulinzi wa jamii zote, ikiwa ni pamoja na Rohingya.

Taarifa iliyotolewa na Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa “Udhaifu mkubwa wa watu katika maeneo yote ya nchi ya Myanmar na athari zake za kikanda zinahitaji jibu la haraka. Kuweza kuwafikia watu wenye uhitaji ni muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa na washirika kuendelea kutoa huduma mashinani. Wanajeshi na washikadau wote lazima waheshimu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi. Watu wa Myanmar wanahitaji kuona matokeo madhubuti.” 

Wakimbizi wa kabila la warohingya wakivuka mpaka karibu na eneo la Anzuman kijiji cha Para, Palong Khali, Bangladesh
© UNHCR/Roger Arnold
Wakimbizi wa kabila la warohingya wakivuka mpaka karibu na eneo la Anzuman kijiji cha Para, Palong Khali, Bangladesh

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu Noeleen Heyzer amekuwa akiwashirikisha wadau wote katika kuunga mkono mchakato unaoongozwa na Myanmar imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa “ Ataendelea kuhamasisha hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN) kushughulikia mahitaji yalitokatiwa tamaa na watu wa Myanmar.” 

Wamebainisha hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kujenga mazingira wezeshi kwa mazungumzo jumuishi. Suluhu yoyote inahitajika kupatikana kutokana na kujihusisha moja kwa moja na kusikiliza kwa makini wale wote walioathiriwa na mgogoro unaoendelea. Sauti zao lazima zisikike na kukuzwa.