Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yachukizwa na hukumu dhidi ya Aung San Suu Kyi wa nchini Myanmar

Aung San Suu Kyi  mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ
ICJ/Frank van Beek
Aung San Suu Kyi mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ

UN yachukizwa na hukumu dhidi ya Aung San Suu Kyi wa nchini Myanmar

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet ameeleza kuchukizwa na hukumu iliyotolewa dhidi ya mshauri mkuu wa serikali ya Myanmar Aung San Suu Kyi aliyehukumiwa kifungo cha miaka minne jela na mahakama inayodhibitiwa na jeshi, na kutaka aachiliwe.

Taarifa kutoka Geneva Uswisi inasema mapinduzi yaliyofanywa na jeshi la Myanmar tarehe 1, Februari mwaka huu wa 2021 walimkamata Aung San Suu Kyi, Rais wa Myanmar na wanachama wengine wa chama tawala pamoja na kuwaweka kizuizini zaidi ya wapinzani elfu 10 ambapo mpaka sasa zaidi ya watu 175 wameripotiwa kufa wakiwa kizuizini kwa kile kinachohisiwa kuwa ni mateso. 

Kamishna Bachelet ametoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa watu wote waliowekwa kizuizini kiholela. 

"Kutiwa hatiani kwa wakili wa serikali katika kesi ya uwongo baada ya mashtaka ya aibu yanayoendeshwa kwa siri katika mahakama inayodhibitiwa na jeshi sio chochote bali imechochewa kisiasa," amesema Bachelet nakuongeza kuwa hukumu hiyo "Sio tu imenyima uhuru wake kiholela bali pia inafunga mlango mwingine wa mazungumzo ya kisiasa."

Aung San Suu Kyi alipatikana na hatia ya uchochezi na kuvunja sheria za kupambana na COVID-19. Bado anakabiliwa na mashtaka mengine ya rushwa na udanganyifu katika uchaguzi. 

Tarehe 10 Novemba Than Naing, aliyekuwa waziri wa mipango wa Jimbo la Kayin, na Nan Khin Htwe Myint, waziri mkuu wa zamani wa Jimbo la Kayin, walihukumiwa kifungo cha miaka 90 na 75 kwa tuhuma za ufisadi.

Kamishna huyo wa Haki za Binadamu amesema "Jeshi linajaribu kutumia mahakama kuuondoa upinzani wote wa kisiasa, lakini kesi hizi haziwezi kutoa sura ya kisheria kwa uharamu wa mapinduzi na utawala wa kijeshi. Hukumu hii dhidi ya Aung San Suu Kyi itazidisha kukataliwa kwa mapinduzi, itafanya kuwa na wakati mgumu ikifika wakati wa kufanyika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya amani na ya kisiasa la mzozo huu."

Bachelet pia amelaani vikali shambulio la kikatili lililoripotiwa jana katika Kitongoji cha Kyimyindaing mjini Yangon, ambako vikosi vya usalama vilitumia lori kuwavamia waandamanaji wasio na silaha na kisha kuwafyatulia risasi kundi.

Kamishna Mkuu alionesha wasiwasi kwamba matukio haya yanahatarisha na kuzidisha mivutano na vurugu.