Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN aeleza wasiwasi wake na matukio yanayoendelea nchini Burkina Faso

Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
© Michele Cattani
Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.

Katibu Mkuu wa UN aeleza wasiwasi wake na matukio yanayoendelea nchini Burkina Faso

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu matukio yanayoendelea nchini Burkina Faso.

Taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa Katibu Mkuu Stéphane Dujarric akiwa jijini New York Marekani imesema Katibu Mkuu analaani vikali jaribio lolote la kunyakua mamlaka kwa nguvu ya silaha na kutoa wito kwa wahusika wote kujiepusha na vurugu na kutafuta mazungumzo.

“Katibu Mkuu anaunga mkono kikamilifu juhudi za kikanda za kurejesha haraka utaratibu wa kikatiba nchini humo, Burkina Faso inahitaji amani, utulivu na umoja ili kupambana na makundi ya kigaidi na mitandao ya kihalifu inayoendesha shughuli zake katika baadhi ya maeneo ya nchi.” Amesema Dujarric

Ameongeza kuwa Katibu Mkuu amesisitiza kujitolea  na ushirikianao wa Umoja wa Mataifa na wananchi wa Burkina Faso katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu wa kudumu.

Hapo jana Septemba 30, 2022 duru mbalimbali za habari za kimataifa zilieleza Rais aliyekuwepo madarakani amepinduliwa na jeshi, ikiwa ni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu tangu Rais huyo ambaye pia ni mwanajeshi kushika madaraka baada ya kufanya mapinduzi mwezi Januari mwaka huu.