Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zidisheni shinikizo kwa jeshi Myanmar likomeshe ukatili - Michelle Bachelet

Waandamanaji walioshiriki matembezi kupinga mapinduzi ya kijeshi Myanmar
@ UNSPLASH/Pyae Sone Htun
Waandamanaji walioshiriki matembezi kupinga mapinduzi ya kijeshi Myanmar

Zidisheni shinikizo kwa jeshi Myanmar likomeshe ukatili - Michelle Bachelet

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameitaka jumuiya ya kimataifa kuzidisha shinikizo kwa jeshi la Myanmar ili likomeshe kampeni yake ya ukatili dhidi ya watu wa Myanmar na kusisitiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia mara moja.

Bi Bachelet amesema, "ninaziomba serikali katika kanda hii na kwingineko kusikiliza ombi hili. Ni wakati wa juhudi za haraka na mpya za kurejesha haki za binadamu na demokrasia nchini Myanmar na kuhakikisha kwamba wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa utaratibu wanachukuliwa hatua.” 

 

Bi. Bachelet ameripoti kwamba wiki hii amezungumza ana kwa ana na watetezi wa haki za binadamu "waliodhamiria, jasiri" ambao wanasihi jumuiya ya kimataifa isiwaache, lakini ichukue hatua madhubuti kuhakikisha haki zao zinalindwa na kwamba jeshi linawajibishwa. 

Mkuu huyo wa haki za binadamu amesema amesikia habari za kutisha za ukiukaji wa haki, kama vile waandishi wa habari kuteswa; wafanyakazi wa kiwandani kutishwa, kunyamazishwa na kunyonywa; na kuzidisha mateso dhidi ya makabila madogo na ya kidini, wakiwemo Warohingya. 

Ripoti nyingine zilitaja kukamatwa kiholela, kuwekwa kizuizini na kesi za kubambikiwa wapinzani wa kisiasa; kwa kutumia kinachojulikana kama "operesheni za kusafisha" zinazolenga wanavijiji; na mashambulizi ya kiholela yakiwemo mashambulizi ya anga na matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye watu wengi. 

Pamoja na hayo, "watetezi wa haki za binadamu wenye ujasiri na wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi wanaendelea kuandamana, kutetea, kuandika na kukusanya ushahidi unaoongezeka wa ukiukaji wa haki za binadamu." Amesema Bi. Bachelet.  

Maoni, kuwekwa kizuizini na kifo 

Tangu jeshi lilipochukua mamlaka mwezi Februari mwaka jana, vikosi vya usalama nchini Myanmar vimejaribu kuzima upinzani, na kusababisha vifo vya watu 1,500: idadi ambayo haijumuishi maelfu ya waliouawa katika vita na ghasia ambazo zimeongezeka nchini kote. 

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imekusanya ushahidi wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kila siku, hasa unaofanywa na vikosi vya usalama. 

Takriban watu 12,000 wamewekwa kizuizini kiholela kwa kutoa maoni yao dhidi ya jeshi, ama katika maandamano ya amani au mtandaoni. Takriban watu 8,792 wamesalia kizuizini, na takriban 290 wamekufa wakiwa kizuizini, pengine kutokana na matumizi ya mateso. 

Ripoti ya kina kuhusu hali ya haki za binadamu itachapishwa mwezi Machi. 

OHCHR imesema mapigano ya silaha yameongezeka mara kwa mara na makali, na kuathiri kila sehemu ya nchi. 

Katika maeneo yenye shughuli nyingi zaidi za kijeshi yaani eneo la Sagaing, pamoja na majimbo ya Chin, Kachin, Kayah na Kayin jeshi limekuwa likiziadhibu jamii. Ofisi ina taarifa na imekusanya taarifa za kuchomwa  moto kwa vijiji, ikiwa ni pamoja na maeneo ya ibada na zahanati za matibabu, pamoja na kukamatwa kwa watu wengi, kunyongwa na matumizi ya mateso.