Ninatoa wito kwa serikali ya Myanmar kurejesha mawasiliano ya intaneti kwa wananchi-Mtaalamu wa UN.

24 Juni 2019

Kitendo cha serikali ya Myanmar kuzima mtandao wa mawasiliano ya simu katika miji minane nchini humo kunaweza kuwa na matokeo mabaya kwa haki za binadamu na ufuatiliaji wa hali ya kiutu katika maeneo ya mgogoro ya Rakhine na Chin, ameonya hii leo huko Geneva Uswisi, Yanghee Lee ambaye ni mtaalamu  maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar.

Mtaalamu huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Myanmar Bi. Yanghee anasema, “katika hali hii ambayo hakuna vyombo vya habari na kuna vikwazo vikali kwa mashirika ya kibinadamu katika eneo lililoathirika na mgogoro, ukanda wote uko gizani. Nina hofu kubwa kwa ajili ya wananchi wote kule, kutokana na kukatwa kwa mawasiliano na bila njia ya watu kuwasiliana ndani na nje ya eneo.”

Ripoti za hivi karibuni zinadai ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria za kimataifa vimefanywa dhidi ya wananchi na vikitekelezwa na pande zote mbili zilizoko katika mgogoro kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

Mnamo Juni 20, wizara ya usafirishaji na mawasiliano ya Myanmar ilitoa amri kwa mitandao yote ya mawasiliano ya simu za mkononi chini ya sheria ya mawasiliano ya simu ya mwaka 2013, kuzuia kwa muda huduma ya intaneti. Wizara ilitaja usumbufu kwa amani na huduma ya intaneti kuwa vinatumika kupanga matukio yaliyo kinyume cha sheria.

Kuna taarifa za uhakika kuwa mnamo Juni 19, kundi la Tatmadaw walifanya mashambulizi kwa njia ya helikopta katika maeneo ya mji wa Minbya katikati mwa Rhakhine. Siku iliyofuata, kundi la Arakan Army likairushia risasi meli ya jeshi la maji huko Sittwe na kuua pamoja na kujeruhi askari kadhaa.

Mgogoro kati ya Arakan na Tatmadaw umekuwa ukiendelea tangu mwishoni mwa 2018 huku wananchi wakiwa waathirika wakubwa wa vurugu hizo. Zaidi ya raia elfu 35 wametawanywa na wenginme wengi wakiwemo watoto wameuawa na kujeruhiwa na pande zote mbili zilizoko katiuka mgogoro. Wengine, hususani wanaume wa Rakhine wamepoteza maisha wakiwa chini ya vizuizi vya kijeshi.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter