Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walimu nchini Honduras huwa hatarini wanapoenda kufundisha shuleni

Familia za wahamiaji nchini Honduras wakitembea kuelekea mpaka wa Guatemala
© WFP/Julian Frank
Familia za wahamiaji nchini Honduras wakitembea kuelekea mpaka wa Guatemala

Walimu nchini Honduras huwa hatarini wanapoenda kufundisha shuleni

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema walimu nchini Honduras wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na ghasia za magenge ya wahalifu na sasa walimu wanatambuliwa kuwa moja ya makundi yenye uwezekano mkubwa wa kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Mwanzoni mwa kila mwaka mpya wa shule, wakati maeneo mengine duniani walimu na wanafunzi hufurahia shule funguliwa, walimu wa nchini Honduras taifa dogo lililoko Amerika ya Kati, hali huwa ni tofauti kwani huwa na hofu wakikaa kusubiri maagizo tena si kutoka serikalini bali katika magenge ya wahalifu ya namna ya kuendesha mafunzo kama anavyoeleza mwalimu Horacio Montes, “wavulana huja kila tunapoanza mwaka wa shule, na wanawasiliana nami ili kunijulisha miongozo ambayo watatupa kuhusu uendeshaji wa shule katika mwaka.”

Maisha ya walimu nayo ni magumu kwani wengine hulazimika kutoa hongo ili waende kazini, huku wakitafuta pesa kila mara wanapovuka mipaka isiyoonekana inayotenganisha maeneo ya magenge kama inavyodhibitishwa na Mwalimu mkuu Miguel Lopez wa shule moja huko Honduras, “Kuna wakati tunaweka maisha yetu rehani, na miili yetu katika hatari ili kuwalinda wavulana na mabinti zetu. Tunaweza kusema kwamba ‘tunabeba mzigo’, lakini hatuna ulinzi sisi wenyewe.”

Walimu wa kike wako katika hatari zaidi, kwani wanaweza kulengwa kwa unyanyasaji wa kijinsia na kushambuliwa kama anavyoeleza Alba Flores Mwalimu Mkuu msaidia wa shule ya awali, “Tunatafuta njia za ulinzi sisi wenyewe, kwa ajili ya wenzetu, wanafunzi na, wakati mwingine, kwa wazazi. Daima tutakuwa marafiki zao watoto, tunawapenda, na tunafanya kazi kwa ajili yao”

Uchunguzi uliofanyika mwaka 2016 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR,  Shirika linalowakilisha walimu wa shule wa Honduras Comité Docent , pamoja na Shirika lisilo la kiserikali la Save the Children, ulibainisha walimu kuwa miongoni mwa makundi nchini Honduras ambayo huathirika zaidi na kulazimishwa kuyakimbia makazi yao.

Walimu wa Honduras wanajikuta kwenye mstari wa mbele wa wakimbizi wa ndani ambapo zaidi ya watu 247,000 wameyakimbia makazi yao.

Wadau wa elimu wamekuwa yakifanya kazi pamoja tangu mwaka 2016 kutafuta suluhu za matatizo yaliyokita mizizi ya walimu ili kuwaweka katika kazi zao na jamii zao nyumbani, lakini pale baadhi ya walimu wanapokuwa katika hatari zaidi hupelekwa UNHCR, ambayo inafanya kazi ya kuwahamishia kwenye usalama zaidi ikiwa ni ndani au nje ya Honduras.