Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yapatia wakulima Afghanistan mbegu bora za kuhimili ukame

Mkulima akipanda mbegu kwenye shamba lake huko Kandahar kwa kutumia mbegu bora kutoka FAO
©FAO/Hashim Azizi
Mkulima akipanda mbegu kwenye shamba lake huko Kandahar kwa kutumia mbegu bora kutoka FAO

FAO yapatia wakulima Afghanistan mbegu bora za kuhimili ukame

Ukuaji wa Kiuchumi

Msimu wa upanzi wakati wa majira ya chipukizi ukiwa unakaribia huko nchiin Afghanistan, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO limepatia wakulima mgao wa mbegu bora za ngano ili kuepusha njaa ilIyowakumba mwaka jana kutokana na kuchelewa kupanda mbegu bora wakati wa msimu wa baridi kali. 
 

Mgao wa mbegu bora za mahindi umefanyika kando sambamba na mafunzo ya kilimo bora huko Damani katika jimbo la Kandahar nchini Afghanistan.

Zaidi ya asilimia 70 ya waafghanistani wanaishi vijijini na kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili la Asia, ikielezwa kuwa asilimia 80 ya mbinu za kujipatia kipato ni kupitia kilimo kinachochangia asilimia 25 ya pato la ndani la taifa.

Kutoka ghalani, moja kwa moja ni shambani upanzi wa mbegu unaendelea ambapo FAO inasema zaidi ya wakulima milioni 1.3 walipatiwa kilo 5 za mbegu za ngano zinazohimili ukame huku watu wengine 700,000 wakipatiwa msaada wa fedha kupitia miradi ya kazi kwa malipo au fedha bila masharti.

Richard Trenchard ni mwakilishi wa FAO nchini Afghanistan na anasema,  “tumeweza kuwafikia wakulima kwa kuwapatia mbegu na mbolea. Hii itahakikisha wana chakula na pia ziada ya kuuza sokoni. Na zaidi ya yote uhakika ya kwamba wana mbegu za ubora kwa ajili ya misimu mingine ijayo.”

Kandahar ni moja ya majimbo 31 kati ya 34 yaliyofikiwa na mgao huo wa mbegu bora za ngano nchini Afghanistan ambapo pia wakulima hao walipatiwa mafunzo ya mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija.