Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazingira bora ya biashara Afghanistan yaleta matumaini

Taswira ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul
UNAMA/Fardin Waezi
Taswira ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul

Mazingira bora ya biashara Afghanistan yaleta matumaini

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkakati wa serikali ya Afghanistan wa kupunguza umaskini, kufungua fursa za ajira na kuboresha mazingira ya biashara umeanza kuzaa matunda na kuimarisha sekta binafsi nchini humo. 

Benki ya Dunia imesema mkakati huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2017 umejumuisha hatua kadhaa ikiwemo kupunguza gharama za kuanzisha biashara,kurahisisha upataji mikopo kwa wananchi, kulinda wawekezaji wadogo na kurahisisha mfumo wa ulipaji kodi.

Naibu Waziri wa biashara nchini Afghanistan, Kamila Sediqi ametoa mfano gharama za kupata leseni ya biashara akisema..

“Mafanikio makubwa ni kuwa gharama za kupata leseni imepunguzwa kutoka afghanis 32,000 sawa na dola 423 hadi afghani 100 ambazo ni dola 1.32. Halikadhalika, awali ilikuwa inachukua siku kadhaa mtu kupata leseni lakini kwa sasa ni saa mbili tu mtu anaipata.”

Kutokana na mabadiliko hayo, ripoti mpya ya Benki ya Dunia kuhusu mazingira ya kufanya biashara kwa mwaka 2019, imeiweka Afghanistan katika nafasi ya 167 kati ya nchi 190, ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 183 mwaka huu wa 2018.

Marekebisho ya kiuchumi nchini Afghanistan yanafadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo Mkurugenzi wake Mkazi nchini humo Shubham Chaudhuri anasema nchi hiyo iliyogubikwa na mizozo imefanya mambo mengi katika kukuza biashara kuliko ambavyo watu wengi wanadhania, ingawa hivyo bado kuna safari  ndefu..

“Mabadiliko yaliyofanywa  yanapaswa kudumishwa, na hilo litahitaji kazi kubwa ili kuhakikisha kuwa  hatua hizi za mwanzo zinaongoza hadi mwisho ili wananchi waweze kuyaona.Tuko tayari kushirikiana na serikali. Sisi katika Benki ya Dunia tunashirikiana  moja kwa moja na washirika  wa serikali na wenzetu katika shirika la fedha la kimataifa IFC ambalo linafanya kazi moja kwa moja na sekta binafsi. Sote tunahitaji kushirikiana na kuendeleza mjadala huu.”