Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya ajira itakua taratibu mno mwaka huu 2022 - Ripoti ya ILO

Kijana Idi Nasibu Davis mjasiriamali ajikimu katikati ya changamoto za COVID-19 ukimbizini Uganda
John Kibego
Kijana Idi Nasibu Davis mjasiriamali ajikimu katikati ya changamoto za COVID-19 ukimbizini Uganda

Sekta ya ajira itakua taratibu mno mwaka huu 2022 - Ripoti ya ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la kazi la Umoja wa Mataifa, ILO limeonya mwaka 2022 sekta ya ajira inatarajiwa kukua taratibu na tena bila uhakika kutokana na kuendelea kuwepo kwa janga la COVID-19 ambalo limeathiri soko la nguvukazi ulimwenguni.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya ILO kuhusu mtazamo wa ajira duniani, WESO iliyotolewa leo Geneva Uswisi ikieleza  kuwa kupungua huko kumetokana na kuendelea kuibuka kwa aina mpya za virusi vya COVID-19 kama ile Delta na Omicron.

Ripoti hiyo ya WESO inaonya juu ya kuwa na utofauti mkubwa katika athari baina ya makundi ya wafanyakazi pamoja na nchi. Tofauti hizo zinazidisha kukosekana kwa usawa ndani ya nchi na hata baina ya nchi hali inayodhoofisisha mfumo wa kiuchumi, kifedha na kijamii wa takriban kila taifa, bila kujali hali ya maendeleo.

Uharibifu huu una uwezekano wa kuhitaji miaka mingi kurekebishwa, kwakuhitaji ushiriki mkubwa wa wafanyikazi, mapato ya kaya na kijamii na pia uwepo wa utashi wa kisiasa.