Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani shambulizi dhidi ya walinda amani wa MINUSMA Mali

Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)
MINUSMA/Sylvain Liecht
Walinda amani kutoka Chad wakipiga doria katika mitaa ya Kidal nchini Mali.(maktaba Desemba 2016)

Guterres alaani shambulizi dhidi ya walinda amani wa MINUSMA Mali

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo amelaani shambulio dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa lililotekelezwa Timbuktu na Tessalit.

Katibu Mkuu huyo ameelezea kusikitishwa na taarifa za kifo cha mlinda amani kutoka Nigeria ambaye amefariki kutokana na majeraha kufuatia shambulizi na watu waliojihami wasiojulikana Timbuktu.

Bwana Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa mlinda amani aliyepoteza maisha na pia kwa serikali ya Nigeria huku akimtakia majeruhi mwingine kutoka Nigeria  kupona haraka.

Halikjadhalika taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemnuku akiwatakia afueni ya haraka walinda amani watatu kutoka Chad ambao walipata na majeraha wakati gari lao lilipigwa na kilipuzi huko Tessalit eneo la Kidal.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anakumbushia kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, yanaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Kwa mantiki hiyo bwana Guterres ametoa wito kwa mamlaka nchini Mali kuchukua hatua na kuwachunguza wahalifu na kuwawajibisha mbele ya sheria.

Katibu Mkuu amesisitiza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na watu na serikali ya Mali na kuelezea utayari wake kuunga mkono juhudi za amani na usalama.