Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu mambo ya kufanya kutokomeza saratani  ya shingo ya kizazi

Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.
© UNICEF/Laurent Rusanganwa
Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.

Fahamu mambo ya kufanya kutokomeza saratani  ya shingo ya kizazi

Afya

Ikiwa mwezi huu wa Januari ni mwezi wa kuelimisha kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema saratani hiyo inaweza kuwa ina ya kwanza ya saratani kutokomezwa ulimwenguni iwapo serikali itaongeza huduma za tiba na kinga.

Dkt. Tedros katika ujumbe wake kupitia ukurasa wa Twitter ametaja mambo ambayo serikali zinapaswa kuzingatia kuwa ni  kupanua wito wa utoaji wa chanjo aina ya HPV ambayo inakinga saratani ya shingo ya kizazi.

Halikadhalika kuongeza huduma za uchunguzi, tiba na uangalizi kwa wagonjwa mahututi wa saratani ya shingo.

Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi
PAHO/WHO
Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema saratani ya shingo ya kizazi inazuilika na inatibika.
Ikitumia takwimu, WHO inasema saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutokomezwa iwapo asilimia 90 ya wasichana watapatiwa chanjo ya HPV kabla ya kutimiza umri wa miaka 15, asilimia 70 ya wanawake wanafanyiwa uchunguzi wakiwa na umri wa miaka 35 na kisha 45, na asilimia 90 ya wanawake wanaobanika kuwa na saratani hiyo wanapatiwa matibabu.

Shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, IARC ambalo ni shirika tanzu la WHO linasema saratani ya shingo ya kizazi ni aina ya pili ya saratani inayopata wanawake ikisababisha pia vifo hasa katika nchi zenye kiwango cha chini ya maendeleo.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2020 pekee, wanawake 604,000 duniani kote walibainika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na kati yao hao 342,000 walifariki dunia.

Kwa sasa IARC na WHO wanashirikiana na wadau wengine kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi kupitia mkakati wa kimataifa wa kuchangiza kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi.

Kwa kiasi kikubwa saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na virusi viitwavyo Human Papilloma na husambazwa kwa njia ya kujamiiana na mtu ambaye tayari ana virusi hivyo.