Uchungu wa maumivu ya mwana wamfanya mama atamani angaliugua yeye saratani

4 Februari 2019

Katika maadhimisho ya siku ya saratani duniani hii leo, shirika la afya ulimwenguni WHO limeangazia kwa kina saratani ya shingo ya kizazi huku ikisisitiza umuhimu wa kuchunguzwa, kupokea chanjo ya Human Papiloma Virus, HPV na kutokomeza kabisa saratani ya shingo ya kizazi. 

Hii ni sauti ya msichana Laura, anasema aligundulika na saratani ya shingo ya kizazi mwaka 2016 ikiwa katika hatua ya pili na kwa sasa hakuna matibabu.

Msichana huyu ambaye anaonekana kwenye video iliyochapishwa kwenye wavuti wa WHO anasema hakupata chanjo ya HPV.

WHO inasema chanjo hiyo inaweza kuzuia aina nyingi za saratani za shingo ya kizazi na inapendekeza watoto wenye umri wa kati ya miaka 9  hadi 13 wapatiwe chanjo hiyo ya HPV ili kuwakinga dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi.

Mama yake Laura anajuta kuugua kwa mwanae akisema ingalikuwa bora angaliugua yeyé badala ya mwanae akisema angalihalikisha wote wanapata chanjo lakini wakati huo hakuwa na taarifa za chanjo ya HPV.

Nako nchini Tanzania Dkt. Limika Lyatuu ambaye ni mtaalam wa saratani akizungumza katika mahojiano maalum na John Kabambala wa radio washirika KidsTime FM amesema kuwa, "wagonjwa tunaopata mara nyingi ni watu wazima, wanaume na wanawake, watoto pia wapo sio kwa idadi kubwa, hapa kwetu bado hatuna kitengo cga saratani kwa hivyo hatuwezi kuthibitisha kwa asilimia mia moja ugonjwa wa saratani bila vipimo zaidi kwa hiyo tukiwapata tunawapa rufaa kwenda Mwimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi ila vile vile tuna kitengo chetu kwa ajili ya saratani ya kizazi kwa wanawake, na wakigundulika tunawapa rufaa kwenda mwimbili ama Ocean Road kupata matibabu".

Dkt. Lyatuu ameenda mbali zaidi na kutoa ushauri kwa jamii, "tunashauri zaidi vipimo vya awali ili mtu agundulike mapema kwa sababu saratani ikiwa kwenye hatua za mapema inaweza kutubika, kwa hiyo msisitizo ambao tunaweka kwenye jamii ni watu waanze kujichunguza afya mapema  kabla hawajaanza kuugua kwani saratani ikigundulika mapema huwa inatibika, pia kutoa elimu, tunasisitiza elimu kuanzia kwenye shule, sio kusubiri mtu azidiwe aua unakuta wengine wanakwenda kwa miti shamba ikishindikana ndio mtu anakwenda hospitali kwa hiyo vipimo vya mapema vinasaidi katika matibabu".

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter