Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya baadaye yasiyo na saratani ya kizazi: Dhamira ya kwanza ya kipekee kabisa ya kuondoa saratani 

Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.
© UNICEF/Laurent Rusanganwa
Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.

Maisha ya baadaye yasiyo na saratani ya kizazi: Dhamira ya kwanza ya kipekee kabisa ya kuondoa saratani 

Afya

Mkakati wa kimatataifa wa shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO wa kuharakisha kutokomeza Saratani ya Shingo ya Kizazi, umezinduliwa leo hii Novemba 17 mjini Geneva Uswisi ukielezea hatua tatu muhimu ambazo ni: chanjo, uchunguzi na matibabu.

Taarifa ya WHO imeeleza kuwa utekelezaji uliofanikiwa wa mambo yote hayo matatu yaani chanjo, uchunguzi na matibabu unaweza kupunguza zaidi ya 40% ya visa vipya vya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na vifo milioni 5 vinavyohusiana na ugonjwa huo kufikia mwaka 2050. 

WHO imesema maendeleo ya leo yanawakilisha hatua ya kihistoria kwa sababu inaashiria mara ya kwanza kwamba nchi 194 zinajitolea kuondoa saratani kufuatia kupitishwa kwa azimio katika Mkutano wa Afya wa Dunia wa mwaka huu. Kutimiza malengo yafuatayo ifikapo mwaka 2030 kutaweka nchi zote kwenye njia inayoelekea kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi kwani  asilimia 90 ya wasichana katika umri wa miaka 15 wamepewa chanjo kamili dhidi ya saratani ya kizazi, HPV, asilimia 70 ya wanawake katika umri wa miaka 35 na baadaye wakiwa umri wa miaka 45 wamechunguzwa kwa kutumia vipimo vya hali ya juu asilimia 90 ya wanawake wanaotambuliwa na ugonjwa wa kizazi hupata matibabu. Taarifa ya WHO Inasema asilimia 90 ya wanawake waliokuwa na dalili za awali za saratani walitibiwa, na 90% ya wanawake walio na saratani kali ilidhibitiwa.  

Mkakati huu pia uliozinduliwa unasisitiza kuwa kuwekeza katika hatua za kufikia malengo haya kunaweza kuleta faida kubwa za kiuchumi na kijamii. Inakadiriwa kuwa dola 3.20 za kimarekani zitarejeshwa kwenye uchumi katika kila dola iliyowekezwa kufikia mwaka 2050 na zaidi, kwa sababu ya kuongezeka kwa ushiriki wa wafanyakazi wanawake. Takwimu hiyo inaongezeka hadi dola 26.00 wakati faida za afya bora za wanawake kwenye familia na jamii zinapozingatiwa, inaeleza WHO. 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Ghebreyesus anasema, "kuondoa saratani yoyote ingeonekana kuwa ndoto isiyowezekana, lakini sasa tuna vifaa vya gharama nafuu, vyenye msingi wa ushahidi ili kuifanya ndoto hiyo iwe kweli. Lakini tunaweza kuondoa saratani ya shingo ya kizazi kama shida ya afya ya umma ikiwa tutalinganisha nguvu ya zana tulizonazo na azma isiyokoma ya kuongeza matumizi yake ulimwenguni. " 

Saratani ya kizazi ni ugonjwa unaoweza kuzuilika. Inatibika pia ikiwa imegunduliwa mapema na inatibiwa vya kutosha. Hata hivyo saratani hii ya shingo ya kizazi ni saratani ya nne ya kawaida miongoni mwa wanawake ulimwenguni. Bila kuchukua hatua za ziada, idadi ya kila mwaka ya visa vipya vya saratani ya kizazi vinatarajiwa kuongezeka kutoka 570 000 hadi 700 000 kati ya mwaka 2018 na 2030, wakati idadi ya vifo kila mwaka inakadiriwa kuongezeka kutoka 311, 000 hadi 400,000. Katika nchi za kipato cha chini na kati, matukio yake ni karibu mara mbili ya juu na viwango vyake vya vifo mara tatu kuliko vile ilivyo katika nchi zenye kipato cha juu. 

Uzinduzi huo unaadhimishwa na siku ya hatua kote ulimwenguni, wakati wizara za afya, washirika, na wanaopambana dhidi ya saratani wanafanya shughuli za kuboresha ufikiaji wa kinga na matibabu ya saratani kwa wasichana na wanawake. 

Hata hivyo mkakati umezinduliwa wakati wa changamoto. 

Janga la COVID-19 limetoa changamoto za kuzuia vifo vitokanavyo na saratani, pamoja na usumbufu dhidi ya chanjo, uchunguzi na huduma za matibabu; kufungwa kwa mipaka ambayo ilipunguza upatikanaji wa vifaa na ambayo inazuia usafirishaji wa wahandisi wenye ujuzi wa vifaa tiba. Pia vizuizi vipya vinavyowazuia mathalani wanawake kutoka maeneo ya ndani vijijini kusaka tiba katika hospitali za rufaa mijini. Kufungwa kwa shule kumeingilia programu za chanjo katika shule. WHO inazisihi nchi, kwa kadri iwezekanavyo kuhakikisha kuwa chanjo, uchunguzi na tiba vinaweza kuendelea kwa usalama huku kukiwa na tahadhari zote muhimu.  

Dkt Princess Nothemba (Nono) Simelela ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa WHO katika vipaumbele vya kimkakati, anasema, "mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi pia ni kupigania haki za wanawake: mateso yasiyo ya lazima yanayosababishwa na ugonjwa huu unaoweza kuzuiliwa yanaonesha ukosefu wa haki unaoathiri kipekee afya ya wanawake ulimwenguni kote. Pamoja, tunaweza kuweka historia kuhakikisha siku zijazo bila saratani ya kizazi.”