Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP na Impact Hub Kigali wazindua mpango wa kusaidia uvumbuzi wa mfumo wa chakula nchini Rwanda 

Mkulima wa Rwanda akiwa ameshika maharage mkononi baada ya mavuno
© WFP/Fredrik Lerneryd
Mkulima wa Rwanda akiwa ameshika maharage mkononi baada ya mavuno

WFP na Impact Hub Kigali wazindua mpango wa kusaidia uvumbuzi wa mfumo wa chakula nchini Rwanda 

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP na taasisi ya Impact Hub Kigali, IHK ya nchini Rwanda pamoja na wadau wengine kama USAID (BHA) na Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, wamezindua shindano la Mifumo ya Chakula nchini Rwanda walilolipa jina IGNITE kwa lengo la kukuza utatuzi wa ndani ya nchi ili kukabiliana na changamoto za mifumo ya chakula. Mpango huo utatoa usaidizi wa kiufundi na jumla ya dola 300,000 za usaidizi wa kifedha. 

Taarifa ya WFP iliyotolewa hii leo mjini Kigali, Rwanda, imeeleza kuwa shindano hili la Mifumo ya Chakula la IGNITE ni mpango wa kwanza wa aina yake wa kusaidia makambuni madogo mapya ya Rwanda, biashara ndogo na za kati (SMEs) na vyama vya ushirika ili kuongeza suluhisho zao, kuchangia uchumi wakati wa kushughulikia mapungufu tofautitofauti katika mfumo wa chakula. Wito wa kutuma maombi umefunguliwa leo tarehe 05 Januari 2022 na utafungwa tarehe 04 Februari 2022. 

Mpango huo unatafuta suluhu za kiubunifu zinazochangia uhakika wa chakula katika maeneo kama vile kustahimili changamoto, upatikanaji wa chakula salama na chenye lishe bora, uboreshaji wa minyororo ya usambazaji wa chakula, uwezeshaji wa wakulima wadogo, na maendeleo ya uhakika wa chakula kwa wote. Biashara zitazochaguliwa zitakuwa na fursa ya kupokea ufadhili wa ruzuku wa hadi Dola za Marekani 50,000 pamoja na usaidizi wa kuchochea ukuaji kwa miezi 6, ikijumuisha kuuunganishwa na wataalam, washauri na washirika, na usaidizi mwingine maalum ili kushughulikia mapungufu ya biashara. 

Pia WFP inasema shindano hili la Mifumo ya Chakula la IGNITE litaendeshwa kwa wakati mmoja nchini Rwanda, Sudan Kusini na Uganda, na linawezeshwa kwa msaada wa dola za Marekani milioni 2 kutoka USAID. Mpango huo unakuja wakati wa hali mbaya ya uhaba wa chakula katika eneo hilo kutokana na athari za kuongezeka kwa migogoro, mabadiliko ya hali ya tabianchi, majanga ya asili kama ukame, mafuriko, nzige na janga la COVID-19

Mkuu wa WFP IGNITE Innovation Hub kanda ya Afrika Mashariki Bwana Jeremie Pigé anasema, “changamoto kubwa kwa wajasiriamali wengi katika Afŕika Mashaŕiki siyo tu kupata ufadhili, lakini pia msaada wa kiufundi ambao unaendeleza mawazo yao. Kupitia usaidizi huu wa ukarimu wa USAID, tuna imani kwamba tutaweza kuwafikia wafanyabiashara wengi mahiri na wenye vipaji katika kanda ambao wanaweza kuwa wameachwa nyuma.” 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Impact Hub Kigali anaongeza akisema, "kwa shindano hili la Mifumo ya Chakula la IGNITE, tutatoa usaidizi maalum kwa wajasiriamali wa ndani ili kuongeza athari zao katika mfumo wa chakula wa Rwanda. Washiriki watafanyiwa uchunguzi mwanzoni mwa programu na wataweza kuunda safari yao ya kuongeza kasi, ikionesha usaidizi wanaohitaji, kutoka kwa kufundisha wenzao na msaada wa kitaalam kama vile huduma za kisheria au uhasibu, kati ya zingine”.