Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda yatekeleza kwa vitendo mkataba wa wakimbizi

Miaka miwili baada ya jukwaa la kimataifa kuhusu wakimbizi, Rwanda imeonesha kwa vitendo sera yake ya ujumuishi wa wakimbizi na wenyeji wao
UN Video
Miaka miwili baada ya jukwaa la kimataifa kuhusu wakimbizi, Rwanda imeonesha kwa vitendo sera yake ya ujumuishi wa wakimbizi na wenyeji wao

Rwanda yatekeleza kwa vitendo mkataba wa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Miaka miwili imepita tangu kufanyika kwa jukwaa la wakimbizi mwezi Desemba mwaka 2019 jijini Geneva, Uswisi, jukwaa ambalo liliwekea msisitizo utekelezaji wa mkataba huo. Kubwa Zaidi ni ujumuishi wa wakimbizi kivitendo kule ambako wamekimbilia kusaka hifadhi. Rwanda imechukua hatua. 
 

Taifa hilo la maziwa makuu barani Afrika limeonesha njia kwa kuwa na sera zinazojumuisha wakimbizi siyo tu katika elimu bali pia katika njia za kujipatia kipato na hivyo kufungua fursa za wakimbizi kustawi wao na wenyeji wao.

Shambani wakimbizi na wenyeji wajumuika pamoja

Katika kambi ya wakimbizi ya Mugombwa nchini Rwanda wakimbizi wake kwa waume kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wakiwa shambani bega kwa bega na wenyeji wao wanyarwanda. Ushirikiano huu ni sehemu ya ahadi 9 za serikali ya Rwanda ya kuwezesha wakimbizi 10,000 wanaowapatia hifadhi mbinu za kupata kipato, elimu, afya, nishati, mazingira bora na ulinzi.

Miongoni mwao ni Bugenimana Clementine mkimbizi kutoka DRC ambaye anasema, “UNHCR ilituunganisha na jamii wenyeji. Wametupatia ardhi ya kilimo huko Icyerechezo Misizi. Tunalima, tunavuna. Kile tunachopendelea Misizi ni kwamba hatuhangaiki tena kupata chakula na tuna fedha kidogo ya akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye.”

Lakini mambo hayakuwa rahisi mwanzoni kama asemavyo Emmanuel Mukuzeyezu kutoka jamii ya wenyeji akisema, “mwanzoni ilikuwa ni vigumu, lakini serikali ya Rwanda ikatuhamasisha tushirikiane na majirani zetu walioko kambini ili tuanzishe ushirika. Tulichukua sehemu ya ardhi yetu tukawagawia.”

Kauli ya Emmanuel inaungwa mkono na Mushimiyimana Yasinne ambaye pia ni wenyeji waliowakaribisha wakimbizi akisema, “Nimemfahamu Clementine kwa miaka miwili na nusu sasa. Awali ilikuwa vigumu mno, lakini sana sisi ni marafiki, halikadhalika Watoto wetu. Sisi siyo tena wanawake wa kizamani wa kuvutana bali tunatiana moyo ili tusonge mbele.”

Darasani mambo ni mazuri

Wanafunzi wakimbizi na wenyeji wako sambamba madarasani na katika vituo vya kuongeza ujuzi. Iteriteka Moise, mkimbizi huyu kutoka Burundi sasa ni mwalimu hapa kambini Kigeme na anazungumzia ubora wa shule kwa wakimbizi akisema, “nina shahada ya kwanza. Ndio maana nasaidia wengine. Nafundisha Kinyarwanda, Kirundi na Kikongo. Pindi wanafunzi wana mazingira mazuri , wanaketi vizuri na wana hamu ya kusoma. Hata wale watoro wanarejea kwa sababu tuna madarasa mapya. Tutakuwa na intaneti na wanafunzi wetu watakuwa na teknolojia kama wengine duniani.”

Mkimbizi kutoka Burundi ameanzisha biashara ya kutengeneza sabuni baada ya kushinda tuzo ya ubunifu miongoni mwa vijana.
© UNHCR/Samuel Otieno
Mkimbizi kutoka Burundi ameanzisha biashara ya kutengeneza sabuni baada ya kushinda tuzo ya ubunifu miongoni mwa vijana.

Na vipi kuhusu kujipatia kipato? Aniella Nizeyimana, mkimbizi kutoka Burundi hapa Rwanda yeye ni mtengeneza sabuni na anasema, “niliondoka Burundi mwaka 2016 pamoja na mume na Watoto wangu wawili. Sababu ya kuanza kutengeneza sabuni ni kwamba niliona wakimbizi wanahitaji kujisafi na sabuni walizopatiwa hazikutosha. Niliuza kambini na hapa kwa wenyeji. Imefanikiwa kwa sababu watu waliunga mkono wazo langu. Ndoto yangu ni kuanzisha kiwanda cha sabuni na familia yangu iendelee. Mengine yote ni historia.”

Kambi imewekewa taa zinazoangazia jamii nzima

Kambi imewekewa ta ana kuna mwanga na sasa uwepo wa kambi hii una manufaa kama asemavyo Mukahigiro Julienne kutoka jamii ya wenyeji.

“Mafanikio yetu kutoka kambini ni mengi. Tuna uhusiano thabiti. Tunaoana. Tunafanya biashara pamoja. Hizo taa za sola unazoona zipo hapa kwa miaka miwili sasa na hii ina maana kila mwanajamii hapa anapata mwanga. Naishi hapa kilimani na hata nikiwa nyumbani napata mwanga.

Nayana Bose ni afisa CRRF nchini Rwanda, ambao ni mfumo wa kufanikisha utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa wakimbizi na hapa anatoa tathmini ya kile kinachofanyika Rwanda akisema, “ni kuhusu ujumuishaji, ujumuishaji wa wakimbizi katika mifumo yote ya kitaifa. Ni kuhusu kubadili fikra kutoka usaidizi wa kibinadamu na kuwekeza kwa watu katika ngazi zote, na ujenzi wa stadi. Serikali ya Rwanda imetoa ahadi na imejizatiti kuona zote zinatekelezwa.”