Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN  yataka uchunguzi wa mauaji ya raia Myanmar akiwemo mtoto

Martin Griffiths, Mkuu wa OCHA.
UN Photo/Manuel Elías
Martin Griffiths, Mkuu wa OCHA.

UN  yataka uchunguzi wa mauaji ya raia Myanmar akiwemo mtoto

Amani na Usalama

Mamlaka nchini Myanmar lazima zichunguze shambulio hatari la hivi karibuni dhidi ya raia kwenye jimbo la Kayans, amesema hii leo Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura, OCHA Martin Griffiths.

 

Bwana Griffiths ametoa kauli hiyo kupitia taarifa ya OCHA iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani kufuatia ripoti ya kwamba watu 35 akiwemo mtoto mmoja wameuawa kwenye shambuli hilo la Ijumaa. Watu hao walilatolewa kwenye magari walimokuwa wakisafiria na kisha kuuawa na wengine kuchomwa moto.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafanyakazi wawili wa kutoa huduma za kibinadamu kutoka shirika la Save the Children hadi sasa hawajulikani waliko ambapo Bwana Griffiths amesema wafanyakazi hao walikumbwa katikati ya ghasia hizo na gari lao lilishambuliwa na kuchomwa moto.
“Ninalaani vikali tukio hili la kikatili na mashambulizi mengine yote dhidi ya raia nchini Myanmar, mashambulio ambayo ni kinyume na sheria za kibinadamu za kimataifa,” amesema Mkuu huyo wa OCHA.
Amesihi serikali ya Myanmar ifanya uchunguzi wa haraka na wa kina dhidi ya tukio hilo na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.
Lindeni raia dhidi ya mashambulizi
Bwana Griffiths pia ametoa wito kwa jeshi la Myanmar pamoja na vikundi vilivyojihami kuchukua hatua zote kulinda raia akisema “mamilioni ya wananchi wa Myanmar wanahitaij misaada ya kibinadamu. Umoja wa Mataifa na wadau wa misaada ya kibinadamu wako tayari kusambaza misaada nchini kote.”
Kwa sasa Umoja wa Mataifa unaendelea kufuatilia hali ya Myanmar kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwezi Februari mwaka huu wa 2021.
Mapema mwezi huu wa Desemba ,ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ,OHCR ilielezea masikitiko yake kufuatia ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye taifa hilo la barani Asia.
Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville alisema ukiukwaji huo wa kupindukia unaripotiwa katika Maisha ya kila siku ya wananchi, uhuru wao na hata usalama wao sambamba na uhuru wa kujieleza.