Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utalii endelevu unaweza kuzipa jamii za milimani njia ya kufikia ustawi na ushirikishwaji 

Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya
World Bank/Curt Carnemark
Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania kama unavyoonekana kutoka nchini Kenya

Utalii endelevu unaweza kuzipa jamii za milimani njia ya kufikia ustawi na ushirikishwaji 

Tabianchi na mazingira

Utalii endelevu una jukumu muhimu katika kukuza maisha, kupunguza umaskini, na uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya milimani, kwa mujibu wa ripoti mpya iliyozinduliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na shirika la utalii la Umoja wa Mataifa duniani UNWTO katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Milima mwaka 2021. 

Chapisho lililoandaliwa kwa pamoja kati ya FAO, Sekretarieti ya Ushirikiano wa Milimani na UNWTO likiwa na jina Utalii wa milimani - Kuelekea njia endelevu zaidi, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO), linaangazia jukumu la utalii katika maendeleo endelevu ya maeneo ya milimani. Chapisho hili lina mifano ya uvumbuzi, mbinu bora na mipango kutoka duniani kote, pamoja na miongozo ya vitendo na mapendekezo katika muktadha wa kurejesha kwa ubora kwa utalii endelevu wa milimani. 

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu katika hafla ya uzinduzi wa chapisho iliyofanyika mjini Roma, Italia, amesisitiza akisema, “kwa jamii nyingi za milimani, utalii ni riziki yao. Kukuza utalii endelevu wa ikolojia, utalii wa kilimo na utalii wa ustawi kunaweza kusaidia kuzalisha ajira mpya, kuongeza mapato, kujenga uchumi mdogo na kufufua maeneo yenye watu wengi kwa bidhaa na huduma za ndani.” 

Kiongozi huyo wa FAO ameongeza akihimiza kila mtu kufanya kazi kwa pamoja ili kulinda mazingira ya milimani akisema, "fikiria upya na kuunda upya utalii wa milimani kwa manufaa ya jumuiya za milimani, ustawi wa kimataifa na afya ya sayari." 

Naye Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili anasema, "utalii endelevu unaweza kutumika kama kichocheo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya milimani. Utalii unaosimamiwa vyema, unaoendeshwa na jamii huongezeka na kuleta mseto wa mapato ya kaya, huongeza nafasi za kazi na maisha, hutegemeza mifumo ya kitamaduni, hujenga uthabiti na husaidia kuhifadhi na kukuza urithi wa asili na kitamaduni katika maeneo mbalimbali. 

Lengo la siku ya kimataifa ya milima 

Umoja wa Mataifa uliiteua Desemba 11 kuwa Siku ya Kimataifa ya Milima, na FAO kama wakala mkuu wa uratibu wake. Inaadhimishwa kila mwaka, inajenga ufahamu kuhusu umuhimu wa milima kwa maisha, ikionyesha fursa na vikwazo katika maendeleo ya milima na kujenga ushirikiano ambao utaleta mabadiliko mazuri kwa watu wa milima na mazingira duniani kote.