Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bioanuwai ya udongo ina umuhimu mkubwa lakini mchango wake haujapewa uzito unaostahili-FAO 

Wanafunzi wakimwagilia mimea maji kwenye shule ya msingi Laos.
© FAO/Manan Vatsyayana
Wanafunzi wakimwagilia mimea maji kwenye shule ya msingi Laos.

Bioanuwai ya udongo ina umuhimu mkubwa lakini mchango wake haujapewa uzito unaostahili-FAO 

Tabianchi na mazingira

Katika kuelekea siku ya udongo duniani hapo kesho Desemba 5 shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO limesema bayonuai ya udongo ina jukumu muhimu la kuchagia katika uzalishaji wa chakula , kuimarisha lishe, kulinda afya ya binadamu, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi , lakini mchango wake mara nyingi haupewi uzito unaostahili. 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO Maria Helena Semedo amesema, "Bioanuai ya udongo na usimamizi endelevu wa ardhi ni sharti la kufanikisha malengo mengi ya maendeleo endelevu. Kwa hivyo, data na taarifa kuhusu bioanuwai ya udongo, kuanzia kitaifa hadi kiwango cha kimataifa, ni muhimu ili kupanga vizuri mikakati ya usimamizi kuhusu suala  ambalo linajulikana kwa kiasi kidogo". 

Udongo ni mojawapo ya hifadhi kuu za bioanuwai ulimwenguni. Udongo unahifadhi zaidi ya asilimia 25 za kibaolojia za bioanuai ya ulimwengu. Kwa kuongezea, zaidi ya asilimia 40 ya viumbe hai katika mifumo ya ikolojia ya ulimwengu huhusishwa na udongo wakati wa mzunguko wa maisha, imeeleza FAO. 

Vitisho kwa bioanuwai ya udongo 

Jukumu la bioanuwai ya udongo kupitia huduma za mfumo wa ikolojia wanazotoa ni muhimu kwa kilimo na usalama wa chakula. 

Kwa mfano, vijidudu vya udongo hubadilisha mabaki mbalimbali na kuachia lishe ambazo mimea huapata chakula chake. Mabadiliko haya pia ni muhimu kwa udhibiti wa uchafu katika maji. Kwa kuongezea, utofauti wa mchanga unachangia kuboresha udhibiti, kuzuia, au kudhibiti wadudu na vimelea vya magonjwa. 

FAO inasema hata hivyo, jukumu muhimu la bioanuwai ya udongo katika kuhakikisha mifumo endelevu ya chakula inaweza kutishiwa na shughuli za kibinadamu, mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili.  

“Matumizi mabaya ya viuatilifu bado ni moja ya sababu kuu za upotezaji wa bioanuwai ya udongo, na hivyo kupunguza uwezekano wa bioanuwai ya udongo kwa kilimo endelevu na usalama wa chakula. Mifano mingine ni pamoja na ukataji miti, ukuaji wa miji, kuongezeka kwa kilimo, uharibifu wa muundo wa udongo, tindikali ya udongo, uchafuzi wa mazingira, chumvi, moto wa nyikani, mmomomyoko, na maporomoko ya ardhi.” FAO imesema.  

Bioanuwai ya udongo na ustawi wa binadamu 

Bioanuwai ya udongo inasaidia afya ya binadamu, moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kupitia udhibiti wa magonjwa na uzalishaji wa chakula. Bakteria kadhaa za udongo na kuvu hutumiwa kiasaili katika utengenezaji wa mchuzi wa soya, jibini, mvinyo, na chakula na vinywaji vingine. Uhusiano kati ya mizizi ya mmea na bioanuwai ya udongo huiwezesha mimea kutoa kemikali ambazo zinawakinga na wadudu na vichocheo vingine. 

FAO inasema, “tunapokula mimea hii, vimeng’enyo vya mimea hutunufaisha kwa kuchochea mfumo wetu wa kinga na kuchangia udhibiti wa homoni. Vidudu vya udongo pia vinaweza kusaidia kuzuia magonjwa sugu ya kuvimba, pamoja na mzio, pumu, magonjwa ya kinga ya mwili, ugonjwa wa tumbo na msongo.” 

Utatuzi 

Kwa ujumla, kuna ukosefu wa data za kina, sera na hatua juu ya bioanuwai ya udongo katika viwango vya mitaa, kitaifa, kikanda na ulimwengu. Ripoti hiyo inaonyesha umuhimu wa kukuza mabadiliko muhimu ili kujumuisha viashiria vya kibaolojia vya afya ya udongo pamoja na ile ya kimwili na kikemikali.