Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kimataifa ya Afya ya mimea yaadhimishwa kwa mara ya kwanza 

Wakulima nchini Tanzania wanatumia mbegu zilizoboreshwa kwa ajili ya mazao bora.
CIAT/GeorginaSmith
Wakulima nchini Tanzania wanatumia mbegu zilizoboreshwa kwa ajili ya mazao bora.

Siku ya kimataifa ya Afya ya mimea yaadhimishwa kwa mara ya kwanza 

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea, IDPH, ulimwengu ukiadhimisha siku hiyo kwa mara ya kwanza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, limesema mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu zinabadilisha mifumo ikolojia na kuharibu bayonuai huku hali hiyo ikiunda maeneo mapya kwa ajili ya wadudu waharibifu kustawi.  

Aidha FAO imeeleza kuwa, “usafiri wa kimataifa na biashara, ambavyo vimeongezeka mara tatu katika muongo uliopita vimechangia kueneza wadudu na magonjwa.”  

“Afya yetu na afya ya sayari yetu hutegemea mimea.” Imeeleza FAO. 

Mimea ni asilimia 80 ya chakula cha binadamu na asilimia 98 ya oksijeni na bado iko chini ya tishio. FAO inasema gadi kufikia “asilimia 40 ya mazao ya chakula hupotea kutokana na wadudu na magonjwa kila mwaka. Hii inaathiri uhakika wa chakula na kilimo, chanzo kikuu cha mapato kwa jamii za vijijini zilizo hatarini.” 

Umoja wa Mataifa uliipitisha tarehe 12 Mei kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea ili kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu jinsi kulinda afya ya mimea kunaweza kusaidia kutokomeza njaa, kupunguza umaskini, kulinda viumbe hai na mazingira na kukuza maendeleo ya kiuchumi na hivyo wito unatolewa kuchukua hatua za kuilinda mimea.