Mtu 1 anauawa kwenye ajali barabarani katika kila sekunde 24- UN

Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New  York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.
UN News/Vibhu Mishra
Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.

Mtu 1 anauawa kwenye ajali barabarani katika kila sekunde 24- UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kila sekunde 24 mtu mmoja anakufa kwenye ajali ya barabarani! Ndivyo ulivyoanza ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya leo ya siku ya kukumbuka waliopoteza maisha au kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani.
 

Katibu Mkuu anasema katika kuadhimisha siku hii ni wakati wa kutafakari juu ya vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani.

Mtu mmoja katika kila sekundi 24 ina maana watu takribani watatu katika dakika moja na jumla ya watu 72 kwa siku nzima ya saa 24.

“Mwaka huu maudhui yanamulika umuhimu wa kupunguza mwendokasi barabarani ili kuzuia vifo na majeraha, hususan miongoni mwa vijana wa kike na wa kiume pindi wanapokuwa ndio kwanza wameanza maisha yao ya utu uzima,”amesema Guterres akiongeza, “pia waenda kwa miguu na watu wenye ulemavu.”

Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana
UN News
Ajali za barabarani yatajwa kuwa sababu kuu ya vifo vya vijana

Guterres anatoa wito kwa kina nchi, kampuni na raia kusaidia juhudi za kitaifa na kimataifa za kuhakikisha barabara zinakuwa salama zaidi hususan kwenye nchi za kipato cha chini na kati ambako zaidi ya asilimia 90 ya vifo vitokanavyo na ajali barabarani hutokea.

Amesihi pia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuridhia mikataba ya kimataifa ya usalama barabarani na kutekeleza mipango kazi yote ya utekelezaji.

Kwa wahisani, ametoa wito waimarishe michango yao ya kifedha na kiufundi kupitia mfuko wa Umoja wa Mataifa wa usalama barabarani.

Katibu Mkuu amesema “tunapotazamia mkutano wa mwaka ujao wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mbinu za kuimraisha usalama barabarani, hebu na tukumbuke kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya ili barabara zetu ziwe salama. Leo na kila siku tuazimie barabara ziwe salama kwa kila mtu kokote aliko.”

Siku ya kukumbuka waliokufa au waliojeruhiwa kutokana na ajali za barabarani inatokana na azimio namba 60/5 tarehe 1 Desemba mwaka 2005 lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, huku mwaka 2020 Umoja wa Mataifa ukitangaza muongo mmoja wa kuimarisha usalama barabarani kuanzia mwaka 2020 hadi 2030.