Ingawa fursa za mtandao ni muhimu kwa watoto pia zina hatari kubwa:UNESCO

4 Novemba 2021

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga ukatili na unyanyasaji mashuleni na mtandaoni, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO limeonya kwamba ingawa matumizi ya mtandao yanatoa fursa kubwa ya mawasiliano na kusoma pia yanawaweka watoto na vijana katika hatari kubwa ya ukatili na unyanyasaji.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema kwa kutambua umuhimu wa kuwalinda watoto na vijana mtandaoni ndio maana imeweka maudhi ya mwaka huu kujikita na “Kukabiliana na unyanyasaji mtandaoni na mifumo mingine ya ukatili inayohusisha watoto na vijana.”

Bi. Azoulay amesema ukweli ulio bayana ni kwamba kila uchao watoto na vijana wanazidi kutumia muda wao mwingi mtandaoni na janga la COVID-19 limzidisha mwenendo huo.

Mathalani amesema “Katika baadhi ya nchi muda unaotumiwa na watoto kurambaza mtandaoni umeongezeka mara mbili kati ya mwezi Mei 2019 na Mei 2020 na duniani kote asilimia 84 ya wazazi wamesema wanahofia usalama wa watoto wao mtandaoni.”

Ameongeza kuwa ingawa hakuna takwimu za kutosha lakini ushahidi unaonesha kuwa unyanyasaji mtandaoni na mifumo mingine ya ukatili wa kisaikolojia umeongezeka wakati wa janga la COVID-19.

Kwa mfano amesema barani Ulaya "Asilimia 44 ya watoto walionyanyaswa mtandaoni kabla ya janga la COVID-19 wamesema ukatili umeongezeka wakati wa hatua za kusalia majumbani.”

Kwa mujibu wa UNESCO ukatili mtandaoni una athari mbaya kwa maendeleo ya elimu na afya ya akili ya wanafunzi.  

Shirika hilo limesisitiza kuwa ingawa ukatili huo sio katika mifumo ya shule pekee, lakini mifumo ya elimu ina jukumu muhimu katika kuwafundisha wanafunzi jinsi gani ya kutumia mitandao kwa usalama kwenye zama hizi za kidijitali ikiwa ni pamoja na jinsi ya kujiwakilisha mtandaoni, kuheshimu wengine, mbinu za kukabiliana nao, kubaini na kuripoti kuhusu ukatili mtandaoni na la msingi zaidi kujilinda wao na kulinda wengine.

UNESCO inasema maadhimisho haya ya pili ya kimataifa ni "Wito kwa wadau wote wa elimu kuanzia wanafunzi, wazazi, waalimu, malaka za elimu na sekta za teknolojia kutimiza wajibu wao katika kuzuia ukatili mtandaoni kwa ajili ya usalama wa watoto na vijana kote duniani."

Siku hii iliyopitishwa rasmi mwaka 2019 na nchi wanachama wa UNESCO inaadhimisha kila mwaka Alhamisi ya kwanza ya mwezi Novemba.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter