Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANBAT 4 yakamilisha ujenzi na kukabidhi madarasa mawili na vifaa kwa wananchi CAR

Mlinda amani akiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
MINUSCA/Leonel Grothe
Mlinda amani akiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati

TANBAT 4 yakamilisha ujenzi na kukabidhi madarasa mawili na vifaa kwa wananchi CAR

Amani na Usalama

Mbali na jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Africa ya Kati CAR, kikosi cha ulinzi wa amani kutoka Tanzania TANBAT 4 kinachohudumu chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa ujulikanao kama MINUSCA nchini humo , kimeweka mikakati ya kusaidia na kuinua wananchi  wa CAR kielimu kupitia shughuli mbalimbali. 

Katika mkoa wa wa Mambere Kadei  wilaya ya Berberati, sambamba na kutoa ulinzi kwa wananchi TANBAT 4 imekuwa mdau mkubwa wa kusaidia wananchi katika shughuli za kijamii na hivi karibuni wamejenga na kukabidhi vyumba viwili vya madarasa na vifaa vya kufundishia ikiwemo ubao kwa kila darasa na madawati 100. 

Vifaa hivyo na madarasa vimekabidhiwa katika shule ya msingi ya kikatoliki ya Secret Heart of Jesus mkoani humo.

TANBAT4 inasema kukamilika kwa madarasa hayo  kama sehemu ya maendeleo ya miundombinu nchini CAR yatasaidia shule kuongeza wanafunzi  100  zaidi kwa kila muhula. 

Hafla ya kukabidhi madarasa hayo na vifaa  ilihudhuriwa na Kamanda wa kikosi cha MINUSCA ; Luteni Jenerali Daniel Sidiki Traore, Balozi wa Tanzania nchini CAR, Luteni Jenerali mstaafu Paul Ignace Mella, Askofu wa Dayosisi ya Berberati, askofu Dennis Kofi Agbenyadzi pamoja na mamlaka za utawala wa mkoa wa Mambere Kadei. 

Kamanda kikosi wa MINUSCA aliwapongeza TANBAT4 kwa juhudi  zao kwenye kufanikisha ujenzi huo.

Naye Balozi wa Tanzania Luteni Jenerali mstaafu Paul Ignace Mella aliongezea kwa kusema "Kazi iendelee mbele ni kauli mbiu yetu Tanzania na motto huu unaotumika sana na Rais wetu Samia Suluhu Hassan nasi tunamuunga mkono mheshimiwa rais kwa kuendeleza jamhuri ya Afrika ya kati katika elimu."

Mwasham Askofu pamoja na mamlaka za utawala wa mkoa wa Mambere Kadei walitoa shukrani zao za dhati kwa TANBAT4 na MINUSCA kwa ujumla kwa mchango wao wa  kuinua elimu nchini CAR.