Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutofanyika uchaguzi kunachelewesha maendeleo nchini Somalia: UN

Somalia inaendelea kukumbwa na majanga sugu ya kibinadamu, huku mizunguko ya mara kwa mara ya mafuriko na ukame, ikichangiwa mwaka 2020 na nzige wa jangwani na COVID-19.
UNSOM
Somalia inaendelea kukumbwa na majanga sugu ya kibinadamu, huku mizunguko ya mara kwa mara ya mafuriko na ukame, ikichangiwa mwaka 2020 na nzige wa jangwani na COVID-19.

Kutofanyika uchaguzi kunachelewesha maendeleo nchini Somalia: UN

Amani na Usalama

Ucheleweshaji unaoendelea wa mchakato wa uchaguzi nchini Somalia unaendelea kukwamisha maendeleo katika maeneo mengine muhimu na kukwamisha mafanikio ya vipaumbele vya kitaifa zaidi ya uchaguzi. 

Hayo yamesemwa na mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Somalia, James Swan, wakati akizungumza na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.  

Swan ametaja vipaumbele vinavyocheleweshwa kuwa ni pamoja na kurekebisha katiba na sekta ya haki pamoja na kuendeleza ajenda ya maendeleo na mageuzi ya kifedha, ikiwa ni pamoja na kufikia hatua ya Kukamilisha mpango wa nchi maskini zenye madeni makubwa mwaka 2022.

Mwakilishi huyo maalum ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, amesema, “hali ya kibinadamu nchini Somalia bado ni mbaya, ikichangiwa na migogoro, wananchi kuyahama makazi yao na milipuko ya magonjwa. Somalia pia iko inakabiliwa na changamoto ya hali mbaya ya hewa hali inayozidisha dharura za kibinadamu mara kwa mara.”

Amebainisha kuwa “Utafiti unaonesha mpaka kufikia mwaka 2022 Wasomali milioni 7.7 watahitaji msaada wa kibinadamu. Kati ya watu hao Watoto waliochini ya miaka mitano ni milioni 1.2 na wapo hatarini kupata utapiamlo wasipopata matibabu ya haraka." Pia amesema wakimbizi wa ndani wanatarajiwa kufikia milioni 2.9 ikiwa ni idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani duniani.

Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan

Kwa upande wake Mwakilishi Maalum wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, na Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia AMISOM, Francisco Caetano Jose Madeira, ameliambia Baraza hilo kwamba “Kundi la Kigaidi la Al-Shabaab linazidi kuongeza mashambuli na kulivuruga jeshi la nchi hiyo kwa makusudi. Mchakato wa uchaguzi unakuwa mgumu kutokana na kikundi hicho kufanya mashambulizi kwenye baadhi ya vituo vya uchaguzi, mashambulizi ya moto yasiyo ya moja kwa moja dhidi ya ngome za AMISOM na kuongezeka kwa mauaji ya hadharani ya watu wanaofanya kazi na vikosi vya usalama vya Somalia na wafanyakazi wa AMISOM.”

Kwa upande wake, Balozi wa Somalia, Abukar Dahir Osman naye ameliambia Baraza  hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa “kufanya uchaguzi huru na wa kuaminika wa wabunge na rais siku zote imekuwa sera iliyoelezwa ya serikali ya shirikisho la Somalia na katika mambo mengi, kucheleweshwa kwa uchaguzi kumekuwa ni matokeo ya makusudi ya kuhakikisha washikadau wote hawaelezwi tu kuhusu mchakato huo bali wanaukubali ili kuhakikisha uhalali wa utawala baada ya uchaguzi.”

Somalia hivi karibuni ilikamilisha uchaguzi wa viti vyote 54 katika baraza la juu la Bunge la Shirikisho na wanawake 14 hivi karibuni wanatarajiwa kuchaguliwa kushika nyadhifa kama Maseneta, wakiwakilisha asilimia 26 ya Baraza la Juu, hata hivyo hii ni pungufu ya lengo la kuwa na wanawake  asilimia 30 ndani ya bunge.
Uchaguzi wa Bunge la Wananchi unaendelea, huku viti 2 kati ya 275 vikiwa vimekamilika, na uchaguzi wa viti kumi na moja vya ziada umetangazwa kuanza wiki hii.