Ubinafsi wa kampuni wasababisha insulini kusalia kitendawili kwa wagonjwa wa kisukari duniani- WHO

12 Novemba 2021

Kwa wagonjwa wa kisukari, insulini ni kitu muhimu sana katika tiba dhidiya ugonjwa huo, ingawa Umoja wa Mataifa unasema miaka 100 tangu kugunduliwa kwake, bado insulini ni vigumu kupatikana kwa wagonjwa wengi.
 

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO iliyotolewa leo kuelekea siku ya kuelimisha umma kuhusu Kisukari tarehe 14 mwezi huu inaonesha kuna ugumu mkubwa kwa wagonjwa wa kisukari kupata insulini sababu ikiwa bei kubwa, upatikanaji hafifu, kampuni chache zinahodhi uzalishaji sambamba na mifumo dhaifu ya afya duniani.

Akizungumzia ripoti hiyo iliyopatiwa jina Kutimiza ahadi ya miaka 100 ya kuhakikisha Insulini inapatikana kwa kila mtu Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus anasema wanasayansi waliogundua insulini miaka 100 iliyopita, hawakuwa wabinafsi na waliuza hataza ya bidhaa hiyo kwa dola moja tu.

“Hata hivyo kitendo chao cha mshikamano kimevurugwa na ubinafsi wa kampuni zenye thamani ya mabilioni ya dola ambazo zimeweka mazingira magumu kwa homoni hiyo kupatikana kwa urahisi,” amesema Dkt. Tedros.

Amesema WHO kwa sasa inashirikiana na nchi na wazalishaji wa Insulini ili kuziba pengo la sasa na kuhakikisha inapatikana ili kuokoa maisha kwa wale wanaohitaji.

Kazi ya insulini mwilini hasa kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 1 (Type 1) ni kuwezesha kupunguza makali ya ugonjwa huo ilhali kwa wagonjwa wa kisukari aina ya 2 au (Type2) Insulini ni muhimu ili kuzuia uwezekano wa figo na ini kushindwa kufanya kazi, kuepusha upofu na kukatwa mguu.

Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa mtu 1 kati ya 2 wenye Kisukari aina ya 2 hapati insulini.
Hivyo ripoti inatoa mapendekezo ikiwemo kuimarisha uzalishaji wa insulini na usambazaji ili bei iweze kupungua.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter