WHO yazindua mpango mpya wa kukabili ugonjwa wa Kisukari

Waisange Wanvula mwanamke mchuuzi wa samaki ambaye pia anaugua kisukari akiwa kambini nchini Uganda.
UN News/ John Kibego
Waisange Wanvula mwanamke mchuuzi wa samaki ambaye pia anaugua kisukari akiwa kambini nchini Uganda.

WHO yazindua mpango mpya wa kukabili ugonjwa wa Kisukari

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limezindua mpango mpya wa kusongesha harakati za kukabiliana na ugonjwa wa kisukari ikiwemo kusaka tiba kwa wale wote wanaohitaji, ikiwa ni miaka 100 tangu kugunduliwa kwa Insulin.

Uzinduzi huo umefanyika wakati wa mkutano wa dunia wa ugonjwa wa kisukari ulioandaliwa kwa pamoja na WHO, serikali ya Canada kwa msaada wa Chuo Kikuu cha Toronto.

Hatua ya leo inazingatia kile ambacho Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa ni umuhimu wa kuchukua hatua hivi sasa dhidi ugonjwa wa kisukari ni dhahiri kuliko wakati wowote ule, "idadi ya wagonjwa wa kisukari imeongezeka mara nne katika miongo minne iliyopita. Ni ugonjwa pekee usio wa kuambukiza ambao hatari ya kufa mapema inaongezeka kuliko kupungua. Na idadi ya wagonjwa mahututi hospitali wenye COVID-19 wana kisukari."

Dkt. Tedros amesema mpango huo mpya utasaidia kuchagiza utashi wa kisiasa katika kuongeza upatikanaji na ufikiaji wa matibabu kwa wagonjwa sambamba na taratibu za uchunguzi na kinga.

Akizungumzia hoja hiyo, Waziri wa Afya wa Canada, Patty Hadju amesema "Canada ina historia ya kujivunia katika utafiti na ubunifu dhidi ya ugonjwa wa kisukari, kuanzia ugunduzi wa Insulin mwaka 1921 hadi miaka 100 baadaye, tunaendelea kufanya kazi na kusaidia watu wanaoishi na Kisukari. Lakini hatuwezi kukabili kisukari peke yetu, tunahitaji kubadilishana ufahamu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kusaidia watu wenye kisukari kuishi muda mrefu zaidi, maisha yenye afya siyo tu Canada bali ulimwenguni kote."

Mhudumu wa afya akimchunguza mgojwa wa kisukari kiwango cha sukari mwilini
WHO/A. Loke
Mhudumu wa afya akimchunguza mgojwa wa kisukari kiwango cha sukari mwilini

Hatua za dharura zahitajika Insulin ipatikane kwa unafuu

Moja ya maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi haraka ni kuongeza upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi wa kisukari na dawa hususan Insulin hasa katika nchi za kipato cha chini na katil.

WHO inasema kuwa kuanzishwa kwa mradi wa majaribio wa kusaka uthibitisho wa uzalishaji wa Insulin mwaka 2019 imekuwa ni hatua muhimu. Hivi sasa soko la Insulin linahodhiwa na kampuni tatu tu. Kufanikiwa kwa mpango wa uthibitisho wa kampuni zaidi, utawezesha kampuni nyingi zaidi kuzalisha dawa hiyo na hivyo kuongeza upatikanaji wake na pia urahisi wa kupatikana kwa unafuu zaidi.

Shirika la afya linasema uhaba siyo wa Insulin pekee bali pia vifaa vya kupima kiwango cha sukari mwilini.

Malengo ya kimataifa ya kukubaliana

Makubaliano hayo pia yanajikita katika kuchagiza maendeleo kwenye kuweka malengo madogo madogo ya kufikia katika tiba dhidi ya kisukari. Halikadhalika yanaweka bayana gharama na faida za kufikia malengo hayo sambamba na kutoa wito kwa serikali kujumuisha ugonjwa wa kisukari kwenye huduma za msingi za afya kwa upande wa kinga na matibabu, ikiwa ni sehemu ya mpango wa huduma ya afya kwa wote, UHC.

Mkurugenzi wa WHO katika Idara ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dkt. Bente Mikkelsen amesema, "lengo la msingi la makubaliano mapya kuhusu ugonjwa wa kisukari ni kuunganisha wadau wote wa sekta ya umma na binafsi na wagonjwa wa kisukari kupitia ajenda moja ya kuchagiza mwelekeo mpya wa kuwa na suluhu za pamoja. Mwelekeo wa suluhu za pamoja katika COVID-19 unatuonesha kile kinachoweza kufanikiwa pindi sekta mbalimbali zinafanya kazi pamoja kusaka suluhu za dharura ya afya ya umma."