Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unaugua Kisukari na sasa kuna COVID-19, ufanye nini?

Dumsile Mavuso kwa miaka 15 sasa amekuwa akihamasisha watu kuhusu ugonjwa wa kisukari nchini Eswatini
© Diabetes Association Eswatini
Dumsile Mavuso kwa miaka 15 sasa amekuwa akihamasisha watu kuhusu ugonjwa wa kisukari nchini Eswatini

Unaugua Kisukari na sasa kuna COVID-19, ufanye nini?

Afya

Ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ukiendelea kutikisa dunia na katika maeneo mengine yakiwa yamekumbwa na wimbi la tatu, shirika la afya la Umoja wa Mataifa linamulika hatari ya ugonjwa wa kisukari katikati ya janga la Corona.

Mchambuzi wetu si mwingine bali ni Daktari Gojka Roglic kutoka WHO na leo atatueleza iwapo unaishi na Kisukari je una hatari gani mbele ya COVID-19 na unawezaje kujikinga dhidi ya virusi hivyo.

Hali ya Kisukari duniani

Dokta Roglic anasema ugonjwa wa kisukari umeendelea kusambaa duniani kote katika kipindi cha miaka 30 na hivi sasa kuna zaidi ya watu milioni 400 ambao wanaishi na ugonjwa wa kisukari duniani.

“Kwa bahati mbaya takribani nusu yao hawafahamu iwapo wana ugonjwa wa kisukari. Hawajaenda kupima. Na wale ambao tayari wameshapimwa na kubainika, wengi wao hawana dawa au huduma za matibabu wanayohitaji.” Anasema Dokta Roglic.

Janga la Corona limedhihirisha kuwa wagonjwa wa kisukari wako katika hatari zaidi  kuwa mahututi zaidi na hata kufariki dunia wakiugua COVID-19 kuliko watu wasio na kisukari. Kuna aina mbili za kisukari, aina ya 1 na aina ya 2. Lakini aina ya 2 ndio imeshamiri zaidi duniani lakini wale wenye aina ya 1 ndio wako hatarini zaidi kuwa mahututi na kufariki dunia iwapo watapata Corona.

Mkazi huyu wa Ha Nam nchini Vietnam mwenye umri wa miaka 68 akionesha dawa zake za kutibu ugonjwa wa kisukari
© WHO/Quinn Mattingly
Mkazi huyu wa Ha Nam nchini Vietnam mwenye umri wa miaka 68 akionesha dawa zake za kutibu ugonjwa wa kisukari

Ubunifu, mazoezi na lishe bora ni kinga kwa mgonjwa wa kisukari

Janga la Corona na mbinu zake za kujikinga ni changamoto kubwa sana kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari. Msingi mkuu ni mazoezi na mlo au lishe bora jambo ambalo linaweza lisiwe rahisi wakati wa mazingira ya Corona. 

Wagonjwa wa kisukari wanapaswa kuwa wabunifu ya jinsi ya kuendelea na mazoezi wanayopaswa kufanya sambamba na lishe bora ndani ya mazingira ya sasa yenye vizuizi na vikwazo kutokana na COVID-19.

Pamoja na juhudi za wagonjwa wa kisukair, mifumo ya afya nayo inapaswa kuhakikisha kuwa wanaendelea kupata dawa zao kila wakati.

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema katika ukanda wa Afrika, kifo 1 kati ya 5 vya COVID-19 vina uhusiano na ugonjw awa Kisukari.
WHO
Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema katika ukanda wa Afrika, kifo 1 kati ya 5 vya COVID-19 vina uhusiano na ugonjw awa Kisukari.

Lakini usalama wa wagonjwa hao ni upi katikati ya COVID-19?

Kwa kuzingatia kuwa wagonjwa wa kisukari wanatambuliwa kuwa wako hatarini zaidi kuugua zaidi kuliko watu wasio na kisukari, “tunapendekeza sana wazingatie hatua zote za kudhibiti kusambaa kwa COVID-19. Hatua hizo ni pamoja na kunawa mikono, kuvaa barakoa, kuhakikisha vyumba wanamoishi vina hewa ya kutosha, kuchangamana na watu maeneo ya wazi badala ya ndani na kuzingatia umbali unaopaswa."
Halikadhalika kuna chanjo ambazo zimeshapendekezwa na wagonjwa wa Kisukari ni kundi la kipaumbele.

Chanjo zinasisitizwa na zimethibitishwa kutokuwa na madhara. Chanjo ni salama na fanisi.