Skip to main content

Malipo kwa wahudumu wa afya Afghanistan yaleta matumaini kwa mamilioni:UN

Mkunga akimuhudumia mtoto mchanga katika kituo cha afya cha familia huko Daikundi, Afghanistan
© UNFPA Afghanistan
Mkunga akimuhudumia mtoto mchanga katika kituo cha afya cha familia huko Daikundi, Afghanistan

Malipo kwa wahudumu wa afya Afghanistan yaleta matumaini kwa mamilioni:UN

Msaada wa Kibinadamu

Wakati kundi la Taliban lilipochukua mamlaka nchini Afghanistan katikati ya mwezi wa Agosti, katika hospitali kuu ya Maidan Shar, jiji lenye wakazi takriban 35,000 katikati mwa nchi hiyo, wafanyakazi wengi walikuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi kadhaa.  

Na vifaa muhimu kama vile dawa na chakula vilikuwa haba, na hata vilipopatikana vilitoweka haraka limesema shirika la Umoja wa Mastaifa la mpango wa maendeleo UNDP

Limeongeza kuwa na usaidizi wote wa kimataifa ulisimama, na ilionekana hakika kwamba kwa wafanyikazi wa afya katika vituo vya kuokoa maisha kwenye taifa hilo lililokumbwa na janga la vita, mamilioni  ya watu wanaowahudumia, mambo yangezidi kuwa mabaya zaidi. 

Lakini kama anavyokumbuka mkunga mmoja katika ushuhuda alioutoa kwa UN News, msaada ulianza kuja, kutokana na makubaliano mapya ya msingi yaliyoongozwa na shirika la UNDP 

Mtoto akipatiwa chanjo ya Polio huko Kandahar, Kusini mwa Afghanistan (Maktaba)
© UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto akipatiwa chanjo ya Polio huko Kandahar, Kusini mwa Afghanistan (Maktaba)

Mkombozi kwa familia 

Katika wiki chache zilizopita, shirika la UNDP, chini ya makubaliano na Mfuko wa Kimataifa Global Fund, wameongeza kwa njia ya kimya kimya msaada kwenye mfumo wa afya wa Afghanistan na familia zote zinazoutegemea, na kutoa dola milioni 15 ili kuepuka kuporomoka kabisa kwa mfumo mzima wa sekta ya afya. 

"Tumeweza kuokoa maisha ya wagonjwa wengi mahututi, na tumeweza kusaidia huduma za wagonjwa, kwa zaidi ya wanawake na watoto 500", amesema naibu mwakilishi mkazi wa UNDP nchini Afghanistan Surayo Buzurukova. 

Huku hali ya hewa ikibadilika kutoka joto la vuli hadi majira ya baridi kali, mmoja wa wakunga anasema alitumia baadhi ya mshahara ambao alikuwa ameanza kupokea hatimaye, kupata mablanketi na vifaa vingine ili kuiweka familia yake salama. 

Mkunga huyo ni mmoja tu wa wafanyakazi wa afya zaidi ya 23,000, katika vituo vya afya karibu 2,200 kwenye mikoa 31, ambavyo vimepokea mishahara tangu mpango huo uanze. UNDP pia imelipia dawa na vifaa vya afya.

"UNDP imechukua changamoto hii kubwa kusaidia kuzuia kuporomoka kabisa kwa mfumo wa afya", amesema Buzurukova. “Bila shaka, haitatui matatizo yote, tunatoa suluhisho la muda. Lakini linasaidia. Tunatuma ujumbe wa matumaini kwa watu wa Afghanistan kwamba sio kila kitu kimepotea, na kwamba hawajasahaulika. 

Changamoto ya miundombinu 

Kwa mujibu wa UNDP, hii inawakilisha kifurushi kikubwa cha msaada wa kifedha kwa sekta ya afya.  
Kabla ya kufika msaada huo, chini ya asilimia 20 ya vituo hivi vya afya ndivyo vilikuwa vikifanya kazi kikamilifu nchini humo. 

Bi. Buzurukova ameeleza kuwa wafanyakazi wote wa afya ambao wamepata mishahara, walitambuliwa na kundi la mashirika 16 ya kiraia ambayo yanachangia mradi wa Benki ya Dunia, unaojulikana kama Sehatmandi. 

Ili kuondokana na vikwazo vinavyoletwa na uhaba wa ukwasi katika mfumo wa benki wa Afghanistan, shirika hilo limebidi kuchanganya vyombo kadhaa vya kifedha kupata fedha. 

Zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wamepokea mishahara yao moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki, na wale wasio na akaunti za benki, ambao mara nyingi wako katika maeneo ya mbali vijijini , wamepokea malipo kwa pesa taslimu. 

"Wahudumu wa afya waliosalia, na hapa tunazungumzia kuhusu jumla ya watu 25,000, watapokea mishahara yao kufikia Alhamisi wiki hii", amesema Naibu huyo wa UNDP. 

Kuendelea na kazi 

Mkunga akitoa huduma katika kituo cha afya cha familia huko Daikundi, Afghanistan
© UNFPA Afghanistan
Mkunga akitoa huduma katika kituo cha afya cha familia huko Daikundi, Afghanistan


Mamilioni ya Waafghani walio katika mazingira magumu wanaendelea kuwa katika hatari ya kupoteza huduma za msingi za afya na shirika hilo linatumai wengine wanaotoa msaada, pia watajiunga na mbinu mpya ya kufanya huduma za afya zifanye kazi katika nchi iliyokumbwa na janga la vita. 

Bi. Buzurukova amesema kuwa shirika hilo lilikuwa katika mawasiliano ya karibu sana na Shirika la afya duniani (WHO) na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF). 
“Wataendelea na malipo. Tunashirikisha mbinu bora, pia tunashirikisha yale yote tuliyojifunza,” alisema. 

Mishahara ya kila mwezi ya wafanyikazi wa afya wa Afghanistan ni kati ya dola $150 kwa mafundi, watoa chanjo, wafanyikazi wa usimamizi au wauguzi, hadi karibu dola $700 kwa madaktari au madaktari bingwa wa upasuaji. 

Kukiwa na watumishi wa umma wapatao 800,000 wakikosa kulipwa ujira kwa miezi kadhaa, mradi huo pia unafungua milango ya kusaidia makundi mengine ambayo kazi yao ni muhimu katika kufanya nchi iendelee, kama vile majaji na walimu. 

Wananchi wakikosea msaada wa chakula unaosambazwa na WFP katika kituo kimoja huko Herat
© WFP/Marco Di Lauro
Wananchi wakikosea msaada wa chakula unaosambazwa na WFP katika kituo kimoja huko Herat

Suluhisho 

Kukatwa ghafla kwa ufadhili wa kigeni kunatishia uchumi mzima, lakini mashirika mengi ya kimataifa na mataifa yanayotoa misaada, bado yanasita kufanya kazi na mamlaka ya Taliban. 

Mwezi Oktoba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alihimiza jumuiya ya kimataifa "kutafuta njia za kufanya uchumi wa taifa hilo kuibuka tena". António Guterres anaamini kuwa hili "linaweza kufanywa bila kukiuka sheria za kimataifa au kuathiri kanuni." 

Ameongeza kuwa "Lazima tutafute njia za kuunda mazingira ambayo yataruhusu wataalamu wa Afghanistan na watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kuwahudumia watu wa Afghanistan” 

Sasa, mpango wa UNDP unatoa suluhisho linalowezekana, ingawa ni la muda mfupi amesema Bi. Buzurukova. 
“Hatuwezi kushirikiana na mamlaka ambazo hazitambuliki na jumuiya ya kimataifa. Tunataka kutoa msaada moja kwa moja kwa madaktari, kwa wauguzi, ambao wanashughulika na watu, na kuwaunga mkono”, amefafanua. 

Matarajio mapya 

Naibu mwakilishi huyo amesema hivi majuzi alirejea kutoka Mazār-i-Sharīf, mji wa nne kwa ukubwa nchini Afghanistan, ambako alitembelea hospitali ili kujionea athari za mpango huo mpya. Na alipata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wanawake. "Ilikuwa vizuri sana kuona kwamba wanawake wanaendelea na kazi zao", amesema. 

Haki za wanawake ni moja ya maeneo makubwa yanayoutia wasiwasi Umoja wa Mataifa tangu kutwaliwa kwa  kwa madaraka na kundi la Taliban, lakini Bi Buzurukova anaendelea kuwa na matumaini kwa siku zijazo. 
Ziara ya Mazār-i-Sharīf ilikuwa sehemu ya mfululizo wa safari ambazo amechukua tangu Agosti 15. Amesema alifanikiwa pia kuzungumza na watu mitaani, kuingia kwenye nyumba za watu, kukutana na familia, vijana, na wananchi ambao ni wazee. 

"Nilivutiwa kabisa na jinsi walivyo na nguvu na mnepo. Kuna imani katika siku zijazo, kwamba watashinda changamoto zinazowakabili na kwamba kesho itakuja, labda si ya uwepesi, lakini itakuja.” 
 

Maelfu ya familia wameyahama makazi yao kutokana na machafuko Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Maelfu ya familia wameyahama makazi yao kutokana na machafuko Afghanistan

Mgogoro wa kibinadamu 

Miaka arobaini ya vita, majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara, umaskini sugu, ukame na janga la COVID-19, vimewaangamiza watu wa Afghanistan. 
Ongezeko la hivi majuzi la mzozo na msukosuko uliotokea umezidisha zaidi mahitaji na kutatiza muktadha wa watu wa taifa hilo wenye changamoto nyingi. 
Hata kabla ya tarehe 15 Agosti, hali ya kibinadamu Afghanistan ilikuwa mojawapo ya hali mbaya zaidi duniani. 

Kufikia katikati ya mwaka, karibu nusu ya idadi ya watu, wote ambao ni watu milioni 18.4, walikuwa tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. 
Mmoja kati ya Waafghanistan watatu walikuwa wakikabiliwa na hali mbaya au viwango vya dharura vya uhaba wa chakula na zaidi ya nusu ya watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano, walitarajiwa kukabiliwa na utapiamlo mkali. 
Hatari za ulinzi na usalama kwa raia, haswa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, pia zilifikia kiwango cha juu. 
Ombi lililozinduliwa mwezi Septemba na Katibu Mkuu linahitaji dola milioni 606 ili kuepuka njaa na magonjwa. Hadi sasa, limefadhiliwa kwa asilimia 54 pekee.