Sekta ya mitindo ya nguo yatangaza mkakati kulinda tabianchi

8 Novemba 2021

Sekta ya ubunifu wa mitindo ya mavazi imetangaza hatua yake ya kuelimisha wazalishaji na wavaaji wa nguo dunia ili waweze kuvaa mavazi yao tena na tena kama njia ya kupunguza uzalishaji na ununuzi wa nguo kupitiliza ambao unachangia katika madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP, sekta ya mitindo ya mavazi ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika janga la tabianchi na ekolojia na linatoa asilimia kati ya 2 hadi 8 ya hewa chafuzi.

Hatua ya leo ni matokeo ya mashauriano yaliyoitishwa na Sekretarieti ya mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC na kutangazwa leo wakati wa mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 huko Glasgow, Scotland na yanazingatia ahadi kuu iliyotolewa na sekta ya mitindo ya mavazi kupitia,  Chata ya sekta ya mitindo ya mavazi kwa hatua dhidi ya tabianchi  ya mwaka 2018 ambayo imefanyiwa  marekabisho.

Uzalishaji wa nguo umeongezeka maradufu katika miaka ya 15 ya mwanzo ya karne hii ya 21 huku kiwango cha urudiaji wa nguo kabla ya kutupwa kimepungua kwa asilimia 36.

Utafiti uliofanywa kwa niaba ya UNEP juu ya mzunguko wa nguo moja umeonesha kuwa kiwango kidogo cha urudiaji wa nguo kimechangia asilimia 24 ya hewa chafuzi kutoka sekta hiyo ya nguo na kwamba kuongeza muda wa kuvaa nguo kabla ya kuitupa kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafuzi, ikimaanisha uzalishaji utapungua kwa kuwa mahitaij ya nguo mpya yatapungua, vivyo hivyo uzalishaji.

Kiwango kidogo cha urudiaji wa nguo kimechangia asilimia 24 ya hewa chafuzi kutoka sekta hiyo ya nguo- UNEP

UNEP inasema iwapo mwelekeo wa sasa wa uzalishaji na uvaaji wa nguo utaendelea, kuna uwezekano mkubwa wa kutofikia lengo la kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwenye sekta hiyo kwa asilimia 50 ifkapo mwaka 2030.

Kampuni 160 zimetia zimekubali kubadili mbinu ya mawasiliano kuanzia kwa wazalishaji hadi wavaaji ili kwenda sambamba na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Uvaavyo nguo unaweza kulinda au kubomoa tabianchi

Steven Stone, Naibu Mkurugenzi idara ya Uchumi UNEP anasema, “kushughulikia suala la matumizi au uvaaji wa nguo ni sehemu kuu ya kupunguza athari za tabianchi kuanzia kiwango cha bidhaa mpya za nguo zinazonunuliwa hadi kiwango cha hewa ya ukaa inayozalishwa sambamba na jinsi ya kutumia bidhaa hizo. Lazima tushirikiane kuwapanga wadau wote pamoja wa sekta hii ya mitindo ya mavazi ili kufikia lengo la kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi kwa mujibu wa mkataba wa Paris.”

Kwa upande wake Lucy Shea ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya mitindo ya mavazi, Futerra amesema “nyanja ya mitindo ya mavazi ni moja ya sekta ambazo zina nguvu sana katika matangazo ya biashara na kusaka masoko. Kile ambacho kampuni, wabunifu na vyombo vya habari vinasambaza vinatoa ushawishi mkubwa katika muonekano wa mtu, anavyojisikia na matendo yake duniani. Kama wapasha habari kutoka kona zote za sekta hii, tunapaswa kuwa pamoja na kutumia nguvu yetu kwa uwajibikaji zaidi ili kushawishi mabadiliko  ya mienendo na tabia ambazo ni muhimu kushughulikia janga la sasa la kibinadamu kwenye tabianchi. Hii ni fursa ya sekta ya mitindo ya mavazi kuwa sehemu ya jawabu, kutumia uwezo wake wa matangazo kuumba maadili mapya na matarajio mapya.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter