Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea mkutano wa tabiachi, jipambanue na vifupisho vya misamiati yake

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kati) na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbambwe pamoja na washiriki wengine wa mkutaon wa kikanda wa Afrika kuhusu maendeleo endelevu, mkutano uliofanyika Zimbabawe.
ECA
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed (kati) na Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbambwe pamoja na washiriki wengine wa mkutaon wa kikanda wa Afrika kuhusu maendeleo endelevu, mkutano uliofanyika Zimbabawe.

Kuelekea mkutano wa tabiachi, jipambanue na vifupisho vya misamiati yake

Tabianchi na mazingira

Kama umekuwa unafuatiliwa Umoja wa Mataifa au UN kwa muda mrefu, bila shaka utakuwa umeshuhudia mlolongo wa vifupisho vya maneno na misamiati migumu ambayo ni nadra kuleta maana kwa msomaji asiyehusika na Nyanja husika. Hii huleta mkanganyiko na hata wakati mwingine mtu kushindwa kufuatilia Habari husika. Tunapoelekea mkutano wa tabianchi huko Glasglow,  Scotland tunaona ni bora kuchambua vifupisho hivyo ili uweze kunufaika na mkutano huo sambamba na taarifa za taifa lako.  

Taka za plastiki katika bahari za ni tisho kwa viumbe wa majini
Saeed Rashid
Taka za plastiki katika bahari za ni tisho kwa viumbe wa majini

COP26 

Hebu tuanze na jina la mkutano wenyewe. Unaitwa COP26 kwa nini? Huu ni mkutano wa 26 wa kimataifa wa nchi wanachama au COP (kwa kiingereza) wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC

UNFCCC ilianzishwa mwaka 1992 wakati wa mkutano wa kimataifa wa mazingira na maendeleo uliofanyika Rio De Janeiro nchini Brazil. Lengo lake lilikuwa kupunguza hewa chafuzi ili kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na shughuli za binadamu. 

Mikutano ya nchi wanachama wa mkataba huo (COP) ni jina rasmi la mikutaon inayofanyika kila mwaka kuanzia mwaka 1995, ukiacha kando mwaka jana 2020 ambao uliahirishwa kutokana na janga la Corona au COVID-19 na sasa unafanyika mwaka huu na hivyo kupatiwa jina COP26. 

SDG 

Kuna malengo 17 yanayoingiliana yakipatiwa jina Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, yanayolenga kusaka suluhusho za changamoto kuanzia za nishati salama, kupunguza umaskini hadi matumzi sahihi ya rasilmali. 

Kwa Pamoja, SDGs zinaunda Ajenda 2030 kwa maendeleo endelevu, nyaraka muhimu ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wakazi wote wa dunia. Inazidi kuwa dhahiri kuwa mabadiliko ya tabianchi yana nafasi kubwa katika takribani malengo yote na kwamba kufanikisha SDGs hakutawezekana bila kuchukua hatua makini katika suala la tabianchi. 

Nzambi Matee, mwanzilishi wa Gjenge Makers ambayo inatengeneza matofali kutokana na taka za plastiki.
UN News/Grece Kaneiya
Nzambi Matee, mwanzilishi wa Gjenge Makers ambayo inatengeneza matofali kutokana na taka za plastiki.

NDC 

Hii ni mipango ambayo kila nchi inajiwekea ili kupunguza utoaji wa hewa chafuzi, kwa kiingereza ni  Nationally Determined Contribution, NDCs. Kila nchi wakati wa mkutano wa 21 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi (COP21) mwaka 2015 walipitisha mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na iliridhia kuandaa mipango hiyo. 

Hata hivyo mipango hiyo haijatosheleza kuweka ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 2 katika kipimo cha Selsiyasi kiwango ambacho ni cha kabla ya mapinduzi ya viwanda duniani. Kwa hiyo mwaka huu nchi lazima zirejee katika meza ya mazungumzo zikiwa na viwango vipya. Bado inaonekana lengo hilo liko mbali. 

Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.
Unsplash/Maxim Tolchinskiy
Uchafuzi wa hewa kutoka kwa viwanda unachangia katika kuongeza nyuzi joto.

Uzalishaji sifuri 

Kwa kiingereza, Net Zero. Inamaanisha nchi haziongezi hewa mpya chafuzi angani: hewa chafuzi zilizoko angani zifyonzwe kiwango hicho hicho duniani. 

Kivitendo, kila nchi imejiung ana mkataba wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi ambayo yanataka ongezeko la kiwango cha joto kisizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi. Iwapo nchi zitaendelea kutoa hewa chafuzi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi, joto litaongezeka na hii itatishia Maisha na mbinu za kujipatia kipato kwa watu wote kila mahali. 

Na ndio maana kuna idadi kubwa ya nchi zinatoa ahadi za kutozalisha hewa chafuzi, ‘Net Zero’ katika miongo michache ijayo. Ni jukumu kubwa linalohitaji hatua thabiti kuanzia sasa. 

1.5°C

Utakuwa unasikia sana katika mkutano huo ‘lengo ni nyuzi joto 1.5  katika kipimo cha Selsiyasi (1.5°C). Mwaka 2018 maelfu ya wanasayansi na wawakilishi wa serikali walitathmini kuwa kuweka ukomo wa ongezeko la joto duniani usizidi nyuzi joto 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda duniani itasaidia kuepuka janga baya zaidi la tabianchi na hivyo kuishi katika mazingira bora. 

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zaidi, kiwango cha joto duniani ni kati ya nyuzi joto 1.06 hadi 1.26  katika kipimo cha Selsiyasi, ikiwa ni juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda mwaka (1850–1900) na kwa mwelekeo wa sasa wa utoaji wa hewa ya ukaa, kiwango cha joto kitakuwa nyuzi joto 4.4 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwishoni mwa karne hii. 

Hii ina maana “janga la tabianchi” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huku kukiwa na uwezekano wa kusambaratika kwa mifumo ya kiekolojia na maisha ya binadamu. 

Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati a
Kadir van Lohuizen/NOOR/UNEP
Tathimini mpya kuhusu mabadiliko ya tabianchi iliyofanywa na jopo la kimataifa la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC imesema Matumbawe yanaweza kupungua kwa asilimia 70 hadi 90 ikiwa kuongezeka kwa joto duniani kutakuwa kwa 1.5 wakati ambapo matumbawe zaidi ya asilimia 99 yanaweza kuwa yametoweka yote katika ongezeko la nyuzi joto 2.

IPCC 

Hiki ni kifupi cha jopo la kiserikali kuhusu tabianchi, au Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC) na ni chombo cha Umoja wa Mataifa kikiwa na wajumbe kutoka serikali mbalimbali wanachama wa Umoja wa Mataifa na jukumu lake ni kutathmini sayansi na uhusiano wake na mabadiliko ya tabianchi. 

IPCC ilianzishwa mwaka 1988 na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la hali ya hewa duniani, WMO na lile la mazingira duniani ,UNEP na lengo la IPCC ni kupatia serikali katika ngazi zote taarifa za kisayansi kuhusu kile ambacho zinaweza kufanya kutunga sera kuhusu tabianchi. 

Ripoti za IPCC ni taarifa za msingi katika mashauriano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi kama itakavyokuwa katika COP26. Ripoti kuu iliyotolewa na jopo hilo ni ile ya mwezi Agosti ambayo ilielezwa na Katibu Mkuu wa UN António Guterres kuwa ni tahadhari kuu kwa binadamu. 

Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.
UNDP Tuvalu/Aurélia Rusek
Tuvalu ambalo ni taifa la kisiwa kwenye bahari ya Pasifiki liko ukanda wa chini na hatarini zaidi kuzama kutokana na ongezeko la kiwango cha maji ya bahari litokanalo na mabadiliko ya tabianchi.

SIDS 

Hiki ni kifupi cha nchi za visiwa vidogo zinazoendelea au kwa kiingereza, Small Island Developing States. Hili ni kundi la nchi 58 zilizo katika visiwa vilivyo hatarini kumezwa na bahari na mara nyingi huathiriwa sana na hali mbaya za hewa na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo vimbunga, Dhoruba, mvua kubwa, ukame, ongezeko la kina cha bahari na ongezeko la viwango vya aside kwenye bahari. 

Wakati wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka huu wa 2021, viongozi wa nchi za SIDS kutoka Fiji, Tuvalu na Maldives walisema mataifa yao yanakabiliwa na tishio la kutoweka iwapo nchi tajiri zitashindwa kutekeleza ahadi zao za kurejesha mwenendo wa ongezeko la joto duniani. 

Ufadhili kwa tabianchi  

Kwa ujumla, uchangishaji fedha au ufadhili kwa tabianchi, unahusiana na fedha ambazo zinahitajika kutumika kutekeleza shughuli zitakazochangia kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani ili lisiongezeke  kwa nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kutoka viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. 

Inaweza kuwa fedha kutoka vyanzo vya kijamii, kitaifa au kimataifa ambazo zimetolewa katika fungu la umma, sekta binafsi au mbinu nyingine mbadala za ufadhili wa miradi hiyo. Ufadhili kwa tabianchi ni muhimu katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa sababu uwekezaji mkubwa unahitajika kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafuzi hususan katika sekta zinazoongoza kwa kutoa viwango vikubwa vya hewa  chafuzi. 

Mwaka 2009, wakati wa mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadilko ya tabianchi, COP15 huko Copenhagen, Denmark, nchi tajiri ziliahidi kutoa dola  bilioni 100 kila mwaka kwa nchi maskini il ikuzisaidia ziweze kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza ongezeko la joto kwa siku za usoni. Ahadi hiyo bado haijatimizwa na hivyo ufadhili kwa tabianchi litakuwa moja masuala makubwa ya mjadala wakati wa COP26. 

Chupa hizi za plastiki zilikuwa taka lakini sasa zimegeuzwa pambo na kuoneshwa wakati ngalawa iliyotokana na taka za plastiki na kandambili ilipowasili Mwanza nchini Tanzania.
Fredy Anthony Njeje
Chupa hizi za plastiki zilikuwa taka lakini sasa zimegeuzwa pambo na kuoneshwa wakati ngalawa iliyotokana na taka za plastiki na kandambili ilipowasili Mwanza nchini Tanzania.

ESG 

Kifupisho hiki cha kiingereza Environment, Social and Governance (ESG) kinahusiana na ufadhili kwa tabianchi kikimaanisha uwekezaji endelevu usioaharibu mazingira lakini vile vile kujali jamii na kuzingatia uongozi bora. 

Uwekezaji endelevu unachochewa na kanuni za kikundi cha uwekezaji wajibivu, au PRI, chombo kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kikilenga masoko endelevu yanayochangia ustawi kwa wote. 

Moja ya malengo ya COP26 ni kuleta kwa wingi zaidi sekta ya biashara pamoja katika ESG na kuchagiza mpito wa uchumi wenye uwiano sawa kwa wote duniani. 

SBTi

Hii ni Mfumo wa malengo yanayochochewa na sayansi, kwa kiingereza  Science Based Target initiative. Kampuni ambazo zinajiunga na mfumo huu zinaweka malengo ya utoaji wa hewa chafuzi kwa kuzingatia viwango vya kisayansi na hivyo zinakuwa katika mwelekeo mzuri wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuzifanya ziwe na ushindani zaidi kuelekea kipindi cha uchumi usiozalisha kabisa hewa chafuzi. 

SBTi imekuwa kigezo cha kipimo kibiashara na mashirika yanakuwa na jukumu muhimu la kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na kusaidia kutekeleza ahadi za nchi, NDCs. 

UN News Kiswahili
Mikoko Pamoja yaleta manufaa Gazi Bay

Majawabu yazingatiayo mazingira asilia 

Majawabu  yanayozingatia mazingira asilia ni hatua za kulinda, kusimamia kwa uendelevu na kurejesha mazingira asili au hata kuboresha mfumo ekolojia kwa kushughulikia changamoto zinazokabili jamii yae neo husika kwa maslahi yao, ziweze kupati ustawi au kipato na wakati huo huo zikilinda mazingira. 

Majawabu haya ni muhimu katika sehemu ya dunia kufikia malengo ya mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi: Majawabu hayo ni muhimu katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, na kupunguza hatari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga jamii zenye mnepo dihdi ya hatari za mabadiliko ya tabianchi. 

Mathalani, yanajumuisha mipango ya upandaji miti ambayo inafyonza hewa ya ukaa na husaidia kuepusha mmomonyoko unaoweza kutokana na mvua kubwa na pia kuhifadhi mikoko ambayo hujenga bamba la kiasilia na rahisi dhidi ya mafuriko katika kanda za pwani. 

G20 

Kundi la nchi 20 au (G20) ni jukwaa la nchi zinazoongoza duniani kwa kuwa na uchumi mkubwa: Ni mataifa 19 na Muungano wa  Ulaya. Kundi hili linafanya kazi kushughulikia masuala makuu yanayohusiana na uchumi wa dunia, kama vile utulivu wa kifedha duniani, kupunguza makali ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameeleza bayana kuwa hatua dhidi ya tabianchi lazima ziongozwe na G20 ambazo kwa pamoja zinachangia asilimia 90 la pato dunia, asilimia 75 hadi 80 ya biashara yote duniani na zina theluthi mbili ya idadi ya watu wote duniani. 

Ahadi zao wakati wa COP26 zitakuwa muhimu katika kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na kutokomeza mabadiliko ya tabianchi. 

AGN 

Hiki ni kifupicho cha kundi la mjadala kutoka Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi au kwa kiingereza The African Group of Negotiators on Climate Change (AGN), na kundi hili lilianzishwa huko Berlin, Ujerumani wa kati wa mkutano wa 1 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP1 mwaka 1995. Kundi hili linasimamia maslahi ya nchi za Afrika katika mashauriano yoyote kuhusu mabadiliko ya tabianchi na huzungumza kwa sauti moja. 

GCAA 

Kando ya majukwaa ya kiserikali, nchi, miji, kanda na sekta za biashara na kiraia duniani kote tayari zimechukua hatua kulinda tabianchi. 

Ajenda ya kimataifa ya hatua kwa tabianchi au GCAA ilianzishwa chini ya Ajenda ya Hatua ya Lima Paris, (Lima Paris Action Agenda)  na ilizinduliwa kuchochea kasi ya hatua kwa tabianchi na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mamlaka za mitaa, wafanyabiashara, wawekezaji, mashirika ya kiraia na kusaidia kupitishwa na kutekelezwa kwa mkataba wa Paris.  

GCAA imechochea hatua zisizo za kawaida za wadau mbalimbali na ahadi za kujenga jamii zenye mnepo na endelevu katika ngazi mbalimbali kuanzia kijamii, kitaifa na kimataifa. Hivi saa ina vikundi 77 vikijumuisha zaidi ya majiij 7,000 na serikali za mitaa, pamoja na kampuni binafsi2,000 kutoka nchi 180 na inasaidia kutekeleza hatua bunifu na endelevu duniani kote ili kulinda tabianchi. 

Idhaa ya Umoja wa Mataifa itakuwa inakuletea habari moto moto kutoka COP26 huko Glasgow Scotland. Unaweza kupata taarifa mbalimbali kuhusu mikutano ya COP hapa