Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP26: Hakuna tena maneno matupu, sekta binafsi zajitoa kimasomaso- Carney

Chama cha ushirika cha wanawake kusini mwa Mauritania kinatumia nishati ya sola kuendesha mtambo wa kumwagilia maji kwenye bustani za mboga.
Climate Visuals Countdown/Raphael Pouget
Chama cha ushirika cha wanawake kusini mwa Mauritania kinatumia nishati ya sola kuendesha mtambo wa kumwagilia maji kwenye bustani za mboga.

COP26: Hakuna tena maneno matupu, sekta binafsi zajitoa kimasomaso- Carney

Tabianchi na mazingira

Katika siku inayomulika sekta ya fedha na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 huko Glasgow, Scotland, takribani kampuni binafsi 500 zimekubaliana kutenga dola trilioni 130 kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ikiwemo hakikisha kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzijoto 1.5  katika kipimdo cha Selsiyasi. 

Mark Carney ambaye ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hatua kwa tabianhi na fedha ametangaza hatua hiyo baada ya kikao alichoitisha huko Glasgow akileta Pamoja kundi la wataalamu wa masuala ya benki, bima na wawekezaji ambao wameahidi kuzingatia mabadiliko ya tabianchi katika kazi zao. 

Je makubaliano haya yana maana gani? 

“Ujumbe mkuu hii leo ni kwamba fedha zipo, fedha zipo katika kipindi hiki cha mpito na siyo tu ‘longolongo’” amesema Bwana Carney akizungumza na wajumbe wakati wa mkutano huo. Gavana Mkuu huyo wa zamani wa Benki ya Uingereza amesema anaona kutozalisha kabisa hewa ya ukaa kuwa ndio jambo muhimu katika mfumo mpya wa fedha. 

“Ni suala la kuzingatia mteja, kwenda ambako kitendo cha kutoa hewa chafuzi kitapunguzwa. Kusaidia kampuni ambazo zina mipango ya kupunguza utoaji wa hewa chafuzi ziweze kupata mitaji na zile ambazo hazina mpango wa kupunguza hewa chafuzi zisipatiwe mitaji. Kwa hiyo tunapendekeza kwamba hiyo mipango iwepo,” amefafanua. 

Mark Carney, Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Hatua kwa Tabianchi na Fedha akizungumza kwenye COP26 huko Glasgow, Scotland
UNRIC/Miranda Alexander-Webber
Mark Carney, Mjumbe Maalum wa UN kuhusu Hatua kwa Tabianchi na Fedha akizungumza kwenye COP26 huko Glasgow, Scotland

Ahadi hii inakuja na mwelekeo ambao kwao kampuni husika nyingi zikiwa kampuni kubwa za nchi za magharibi ,zinapaswa kutumia miongozo ya kisayansi kufikia lengo la kutotoa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050 na kuahidi kuwa na malengo ya kati ya kufikia punguzo la utoaji hewa chafuzi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 na hata asilimia 25 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 

Hii ina maana kwamba kurekebisha miundo na mifumo yao ya kibiashara na kuandaa mipango ya kina na halali kwa kipindi cha mpito na kisha kuanza kuitekeleza. 

“Na kisha ripoti muhimu za kila mwaka. Tutapata taarifa za nani anafanya vizuri, nani anapaswa kuongeza bidii na pia kwa upande wa sera, nini kipo na nini hakipo,” ameeleza Bwana Carney. 

Kwa nini tunahitaji sekta binafsi kufadhili tabianchi? 

Kwa mujibu wa ushirika huo, fedha kutoka sekta binafsi inaweza kufadhili mipango ya sekta binafsi na kugeuza mabilioni ya fedha yanayoelekezwa katika vitegauchumi vya tabianchi kupitia sekta ya umma kuwa matrilioni ya fedha katika uwekezaji. Lakini kutoa hizo fedha hizo na mfumo uanze kufanya kazi kunahitaji ushirikiano, ahadi za kina na hatua mtambuka katika mfumo mzima wa fedha. 

“Hadi leo hii hakuna fedha za kutosha duniani kufadhili kipindi cha mpito cha mageuzi; huu ni wakati muhimu,” Bwana Carney amewaeleza wajumbe wa COP26. 

Kwa mujibu wa  Patricia Espinosa, Katibu Mkutendaji wa Sekretarieti ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, (UNFCCC), hakuna shaka kuwa lazima kuwepo na marekebisho ya kina ya mfumo wa uchumi duniani na sekta binafsi lazima iwe sehemu ya mfumo mpya wa uchumi. 

“Sekta binafsi inatambua kuwa hatari zitokanazo na tabianchi zinagusa sana sekta zao na hivyo ni lazima ijipange vyema ili shughuli zifanyike kwa uendelevu zaidi,” amesema Bi. Espinosa wakati akizungumza na waandishi wa Habari. 

Kutumia upepo kuzalisha nishati kuna madhara machache kwa mazingira kuliko vyanzo vingine vingi vya nishati.
© Unsplash
Kutumia upepo kuzalisha nishati kuna madhara machache kwa mazingira kuliko vyanzo vingine vingi vya nishati.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira, UNEP, Inger Andersen amesema ushirikiano huo mpya na sekta binafsi ni hatua nzuri. 

“Ripoti yetu ya pengo la utoaji wa hewa chafuzi inaonesha: kuna takribani tani bilioni 500 za hewa ya ukaa na kwa kuzingatia ahadi za sasa za kitaifa, NDCs za kupunguza hewa hiyo, ni tani bilioni 4 tu ndio zinaweza kutoka angani huku tukitoa tani bilioni 5 kila mwaka. Hesabu hii haikokotoki. Kuna fursa za kihalisia kupitia sekta ya fedha, tunahitaji kuachana na makaa yam awe, mafuta na gesi,” amesema Bi. Andersen. 

Sekta ya Biashara imeitika

Guenther Thallinger, kutoka shirika la Allianz la huduma za kimataifa za kifedha nchini Ujerumani ameelezea azma yao katika ushirika mpya wa taasisi za kifedha uliofikiwa huko Glasgow au Glasgow Financial Alliance.  

“Inaanza na kubadilisha uamuzi wa sisi tulio na taasisi za kifedha. Madhara ya tabianchi lazima yawe sehemu ya hatua zetu za kupitisha uamuzi na ndio maana melngo ya muda wa mpito ni muhimu. Sote tumeweka aina hii ya malengo na ni muhimu sana yanakuwa ya muda mfupi,” Amesema  Thallnger wakati akizungumza kwenye jopo la kikao cha Uchukuaji Hatua huko Glasgow. 

“Ni kwamba tunaanzisha sekta mpya, kanuni mpya ambazo zinapatia kipaumbele hatua kwa tabianchi. Kwa hiyo tunachohitaji vipimo, kutoa taarifa na napenda kuchukua fursa hii kutangaza kuwa tutatoa awamu yetu ya kwanza ya malengo ya mpito,” amesema Audrey Choi, Afisa Mkuu wa Uendelevu kutoka taasisi ya Morgan Stanley.  

Na vipi kuhusu fedha kwa sekta ya umma?   

Wakati wa mkutaon wa COP15 mwaka 2009, kiasi ya dola bilioni 100 kiliahidiwa kutolewa kila mwaka na nchi tajiri kwenda kwa nchi zinazoendelea ili kutekeleza mipango yao ya kuhimili na kujenga mnepo dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa sasa ahadi hiyo imesogezwa mbele hadi mwaka 2023. 

 Hata hivyo, Alok Sharma, Rais wa mkutano wa COP26 ametangaza habari njema: asilimia 90 ya uchumi wa dunia sasa umeweka lengo la kutozalisha hewa ya ukaa. Ni asilimia 30 tu imeahidiwa mwanzoni mwa mwaka 2020. 

“Ni jambo la kusikitisha kuwa kuna uwezekano mdogo wa kufikia lengo la dola bilioni 100 mwaka huu wa 2021, lakini kwa kuzingatia taarifa kutoka kwa wahisani,uchambuzi unaonesha kuwa nchi tajiri zitachukua hatua muafaka ili lengo lifikiwemo mwaka 2022 na ninaamini kuwa tutajengewa imani kuwa litafikiwa mwaka 2023,” amesema Bwana Sharma wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo. 

Mapema akizungumzia suala hilo la utoaji fedha, Rishi Sunak ambaye ni Waziri wa Fedha wa Uingereza amesihi nchi tajiri kuimarisha usaidizi wao kwa nchi zinazoendelea ikiwemo kuzisaidia kupata trilioni za dola za kupunguza hewa chafuzi kutoka sekta binafsi. 

Hata hivyo Mkuu wa UNFCCC Patricia Espinosa amesisitiza kuwa kuna maendeleo katika hatua hiyo akisema, “Marekani imeungana na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Muungano wa Ulaya kwenye ubi ana mabilioni ya dola kusaidia Afrika Kusini kwenye kipindi cha mpito cha kuachana na makaa ya mawe. Mpango huo una thamani ya dol abilioni 8.5. 

Ameongeza kuwa Japan na Australia nazo zimetangaza ahadi zao za kuongeza maradufu ufadhili kwenye mipango ya kuwezesha nchi kuhimili mabadiliko ya tabianchi huku Marekani, Uswisi na Canada nazo pia zikiongeza kiwango cha fedha za usaidizi. 

Picha hii ya tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 2018, inaonesha paneli za sola zinazozalisha umeme wa kusukuma maji katika mtambo uliojengwa na UNICEF huko Yambio , SUdan Kusini.
© UNICEF/Sebastian Rich
Picha hii ya tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 2018, inaonesha paneli za sola zinazozalisha umeme wa kusukuma maji katika mtambo uliojengwa na UNICEF huko Yambio , SUdan Kusini.

Halikadhalika nchi zimeahidi kupeleka dola bilioni 13 kwenye harakati za kuimarisha misitu kati ya mwaka huu wa 2021 hadi 2025. 

“Ahadi mpya zimetangazwa pia na Hispani, Ireland, Luxembourg na hivyo nina matumaini kuwa ifikapo mwishoni mwa mkutano huu tunaweza kupata lengo la dola bilioni 100 mwaka 2022,” amesema Bi. Espinosa.