Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu ya WFP ya mlo shuleni nchini Rwanda yatekeleza malengo 6 ya SDGs

Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.
© FAO/Petterik Wiggers
Wakulima nchini Rwanda na juhudi za kuimarisha ardhi.

Programu ya WFP ya mlo shuleni nchini Rwanda yatekeleza malengo 6 ya SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP nchini Rwanda, linaendesha programu ya chakula kutoka nyumbani kwenda shuleni, programu ambayo inatekeleza malengo 6 ya maendeleo endelevu, SDGs likiwemo namba 2 la kutokomeza njaa na hivyo kuwaacha wazazi na wanafunzi wakiwa na furaha.

Programu hii ya kuwapatia wanafunzi mlo shuleni inatekelezwa katika nchi nyingi duniani na pengine mtu anaweza kujiuliza chakula hicho kinatoka wapi?. Nchini Rwanda programu ya mlo shuleni inayotekelezwa na WFP hununua mazao yanayotumika kwa chakula hicho kutoka kwa wakulima wa maeneo yaliyo karibu na shule.
 
Amy Blaumen, afisa wa WFP akihusika na sera wa programu ya mlo shuleni anasema wapishi ni wazazi halikadhalika mazao yanatoka kwa wazazi.

"Zaidi ya wakulima 10,000 wanaungwa mkono na WFP kupitia program yetu, wakulima wanafundishwa ukulima na utunzaji bora wa mazao baada ya kuvuna na matokeo yake tunatarajia ujuzi huu utawasaidia kuongeza mazao yao, mazao kuwa bora na kuyauza katika shule zilizoko karibu na mashamba yao.” amesema  Blaumen
 
Mfumo huu umeleta mapinduzi makubwa kwenye uimarishaji wa mifumo ya chakula, elimu bora na jamii zinabadilika. Mwanafunzi Elisa ni mnufaika wa program hii ya mlo shuleni. “Natamani wanafunzi wote wangepata chakula shuleni. Kabla ya kuanza kupata chakula shuleni, wanafunzi wengine walishindwa kumakinika darasani, na wengine waliacha shule.“
 
WFP inaendesha program hii ya mlo shuleni inayotumia mazao yanayolimwa na wazazi jirani na shule katika zaidi ya nchi 40.  
 
Wanafunzi wanapata chakula salama na chenye lishe bora, wanatoa fursa kwa wakulima na kupunguza upotevu wa chakula ambayo ni moja ya sababu kubwa za kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni.
 
Malengo mengine yanayofanikishwa na programu ya mlo shuleni ni namba 1 la kutokomeza umaskini, namba 4 kuhusu elimu bora, namba 5 usawa wa jinsia,  namba 8 kuhusu ajira zenye staha na ukuaji wa uchumi na namba 10 linalohusi kupunguza ukosefu wa usawa.