Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unaelewa nini kuhusu fedha kwa kukabili mabadiliko ya tabianchi?

Juhudi za pamoja za kusaidia kupunguza uchafuzi wa tabaka la ozoni zitafanya tabaka hilo lipone kutokana na majeraha ya uchafuzi kwa miongo kadhaa
WMO/Chunseong Bang
Juhudi za pamoja za kusaidia kupunguza uchafuzi wa tabaka la ozoni zitafanya tabaka hilo lipone kutokana na majeraha ya uchafuzi kwa miongo kadhaa

Unaelewa nini kuhusu fedha kwa kukabili mabadiliko ya tabianchi?

Tabianchi na mazingira

Je unaposikia nchi zilizoendelea zinahamasishwa kutoa fedha kufanikisha miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi unaelewa nini?. Je ni nani anasimamia fedha hizo, zinatumika kwenye maeneo gani? nani ananufaika na fedha hizo na uamuzi wa kuanza kuchanga ulitokea wapi?

Ufadhili kwa miradi ya tabianchi

Fedha za miradi ya tabianchi ni fedha zinazotolewa na watu binafsi, taifa au mataifa ambazo zinakusanywa kutoka vyanzo vya umma, binafsi na vyombo mbadala kwa lengo la kusaidia hatua za kupunguza na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. 

Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris vimetaka kuwepo kwa msaada wa kifedha kutoka vyanzo vilivyo na rasilimali nyingi kifedha kwenda kwa wale wenye uwezo mdogo na walioko hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Itifaki hii inatambua kwamba mchango unaotolewa na nchi moja na nyingine kwenye mabadiliko ya hali ya hewa na uwezo wao wa kuzuia na kukabiliana na athari zake hutofautiana sana. Fedha hizo zinahitajika ili kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwasababu uwekezaji mkubwa unahitajika katika kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa. 

Si kuzuia tuu, fedha za mabadiliko ya tabianchi zinahitajika kwa usawa huo huo wa kuzuia kwenye kukabiliana na athari mbaya na kupunguza athari zitokanazo na maadiliko ya tabianchi.

Mkataba wa Paris

Kanuni ya "uwajibikaji wa kawaida lakini uliotofautishwa na uwezo husika" uliowekwa katika Mkataba, nchi zilizoendelea zinapaswa kutoa rasilimali fedha ili kusaidia nchi zinazoendelea katika kutekeleza malengo ya mkataba wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC.. 

Mkataba wa Paris umeeleza wajibu wa nchi zilizoendelea, na kuhimiza michango ya hiari kwa wadau wengine. Nchi hizo zilizoendelea pia zimepewa jukumu la kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia kwenye mabadiliko ya hali ya hewa. Nchi hizo pia zimepewa jukumu la kuunga mkono mikakati inayoendeshwa na zinazoendelea pamoja na kuzingatia mahitaji na vipaumbele vya nchi hizo. 

Ni muhimu kwa serikali na wadau wote kuelewa na kutathmini mahitaji ya kifedha ya nchi zinazoendelea, na pia kuelewa jinsi rasilimali hizi za kifedha zinaweza kuhamasishwa. Utoaji wa rasilimali pia unapaswa kulenga kufikia usawa kati ya kuzuia na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa ujumla, juhudi zilizo chini ya Mkataba wa Paris zinaongozwa na lengo lake kuu la kufanya kuwepo na mtiririko wa kifedha unaoendana na uzalishaji mdogo wa hewa chafuzi kwa tabaka la ozoni pamojana kufanya maendeleo yanayo stahimili hali ya hewa 

Mkataba wa Paris pia unasisitiza juu ya uwepo wa uwazi na utabiri unaoaminika wa msaada wa kifedha.
Utaratibu wa kifedha 

Ili kuwezesha utoaji wa fedha za miradi ya kudhibiti tabianchi, Mkataba ulianzisha utaratibu wa kifedha wa kutoa rasilimali fedha kwa upande wa nchi zilizoendelea kwenda nchi zinazoendelea. Utaratibu huu wa kifedha pia unatumikia kwneye Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Paris.

Mkataba unasema shughuli za uendeshaji wa wa taratibu za kifedha zinaweza kukabidhiwa kwa taasisi moja au zaidi za kimataifa zilizopo.  Kituo cha Mazingira Duniani (GEF) kimekuwa kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha tangu kuanza kutumika kwa Mkataba huo mwaka 1994. Katika Mkutano wa 16 wa nchi wanachama wa UNFCCC, COP16, nchi zilianzisha Mfuko wa tabianchi  (GCF) na mwaka 2011 kuuteua kama chombo cha uendeshaji cha utaratibu wa kifedha. Utaratibu wa kifedha unawajibika kwa COP, ambao ndio unafanya maamuzi ya sera zake, programu zitakazopewa kipaumbele na vigezo vya wakataokuwa wanastahili kupata ufadhili.

Pamoja na kutoa muongozo GEF na GCF zimeanzisha mifumo miwili maalum ya fedha. 
1.    Mfuko Maalum wa Mabadiliko ya Tabianchi (SCCF) 
2.    Mfuko wa Nchi masikini zaidi (LDCF)

Mifuko yote hiyo inasimamiwa na GEF na Mfuko wa Kukabiliana (AF) ulioanzishwa chini ya Itifaki ya Kyoto mnamo 2001.

Fedha za noti zinachapishwa na serikali
Unsplash/Jason Leung
Fedha za noti zinachapishwa na serikali

Kamati ya Kudumu ya Fedha

Katika Mkutano wa COP16, wanachama waliamua kuanzisha kamati ya kudumu ya fedha (SCF) ili kusaidia mkutano huo kutekeleza majukumu yake kuhusiana na utaratibu wa kifedha kama ulivyoamuliwa na Mkataba.

Hivi sasa, kamati hiyo ina kazi nne maalum ya kusaidia nchi wanachama wa UNFCCC, 
1.    Kuboresha mshikamano na uratibu katika utoaji wa fedha za mabadiliko ya hali ya hewa.
2.    Kurekebisha utaratibu wa kifedha wa UNFCCC.
3.    Kuhamasisha rasilimali fedha kwa ufadhili wa tabianchi
4.    Kupima, kuripoti na uhakiki wa msaada unaotolewa kwa nchi zinazoendelea. 
Kamati pia imepewa jukumu la kuandaa mkutano wa kila mwaka juu ya fedha za hali ya hewa, kutoa rasimu ya muongozo wa uendeshaji wa vyombo vya UNFCCC, kutoa maoni ya wataalamu katika ufanyaji wa mapitio ya mara kwa mara ya utaratibu wa kifedha, na kuandaa tathmini ya miaka miwili na muhtasari wa mtiririko wa fedha za tabianchi.

Kwa kuongezea, SCF imeundwa kuboresha uhusiano na kukuza uratibu na watendaji na mipango inayohusiana na fedha za mabadiliko ya tabinachi ndani na nje ya Mkataba. Katika Mkutano wa Paris mnamo 2015, wanachama waliamua SCF pia itatumikia Mkataba wa Paris.

Mipango ya muda mrefu ya fedha za tabianchi

Mchakato wa muda mrefu wa fedha hizi unakusudia kuendelea kuhamasisha na kuongeza fedha za hali ya hewa kutoka kwenye vyanzo vingi tofauti vya umma na vya kibinafsi, mahusiano ya nchi mbili na zaidi, pamoja na vyanzo vingine mbadala.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi uliamua juu ya shughuli zifuatazo hadi kufika mwaka 2020, kuratibu semina za vikao vya kila mwaka, nchi zilizoendelea kutoa taarifa kila baada ya miaka miwili, taarifa juu ya mikakati na njia za kuongeza fedha za ufadhili wa masuala ya tabianchi, na kuitisha mazungumzo ya mawaziri ya ngazi ya juu ya miaka miwili kujadili  kuhusu fedha za tabianchi.

Kupitia Mikataba ya Cancun wa mwaka 2010 nchi zilizoendelea ziliweka ahadi ya kuweka mikakati ya kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na kuwa na uwazi juu ya utekelezaji wa lengo la kukusanya dola za bilioni 100 kila mwaka fedha zitakazotumika kushughulikia mahitaji ya nchi zinazoendelea.

Wakati wa kupitisha Mkataba wa Paris nchi zilizoendelea zilithibitisha kuwa zitatekeleza lengo hilo, na kuweka mpango wa kufikia utekelezaji wa lengo hilo mwaka 2020, na wakakubali kuwa kabla ya mwaka 2025 kutakuwa na mkutano w anchi zilizoendelea ili wanachama wa Mkataba wa Paris (CMA) waweke lengo jipya la pamoja ambalo litaanzia kwenye dola bilioni 100 kwa mwaka.

Watu wanaumia mitandao kuagiza na kulipia bidhaa kote duniani.
ITU/G. Anderson
Watu wanaumia mitandao kuagiza na kulipia bidhaa kote duniani.

 

Wavuti wa taarifa za fedha za tabianchi

Tovuti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa UNFCCC inajumuisha wavuti ndogo yenye takwimu kuhusu fedha za hali ya hewa na maelezo muhimu, pia kuna picha na takwimu za kuelewa vizuri mchakato wa fedha za hali ya hewa na inatumika kama lango la habari juu ya shughuli zinazofadhiliwa katika nchi zinazoendelea kutekeleza miradi ya hali ya hewa.

Wavuti hiyo ndogo imegawanyika katika maeneo matatu ambayo kila moja ina taarifa za zilizotolewa na nchi zinazofadhili, zinazofadhiliwa na vyombo vya uendeshaji wa kifedha.