Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres amteua tena Bloomberg kuwa mjumbe wake maalum wa tabianchi 

Katibu Mkuu Antonio Guterres alipokutana na Michael Bloomberg mjumbe maalum wake wa tabianchi. (Picha ya Maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu Antonio Guterres alipokutana na Michael Bloomberg mjumbe maalum wake wa tabianchi. (Picha ya Maktaba)

Guterres amteua tena Bloomberg kuwa mjumbe wake maalum wa tabianchi 

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua tena Michael Bloomberg wa Marekani kuwa mjumbe wake maalum wa hatua thabiti na zenye matamanio makubwa katika kukabili tabianchi. 

Tangazo la uteuzi huo limetolewa leo jijini New York, Marekani ambapo Bwana Bloomberg atakuwa mhasishaji wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kuelekea mkutaon muhimu wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa tabianchi, COP26 utakaofanyik ahuko Glasgow mwezi Novemba mwaka huu. 

Awali Bwana Guterres alimteua Bloomberg kuwa mjumbe wake maalum katika wadhifa huo tarehe 5 mwezi Machi mwaka 2018, jukumu ambalo aliendelea nalo hadi alipojiuzulu wakati alipotangaza nia yake ya kuwania urais wa Marekani mwezi Novemba mwaka 2019.

Bwana Bloomberg  ataunga mkono kazi za Katibu Mkuu za kusaka na kuimarisha ushirikiano baina ya serikali, kampuni, taasisi za kifedha kwenye kutoa ahadi zao za kutotoa hewa chafuzi kabla yam waka 2050, kwa mujibu wa mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Mathalani atajadilianana serikali na sekta binafsi na mashirika ya kiraia katika kuhitimisha mipango yao ya utekelezaji, hususan kwenye nchi ambazo bado zinaongoza katika utoaji wa hewa chafuzi ili hatimaye zijikite na nishati endelevu na salama. 

“Bwana Bloomberg atatumia uzoefu wake katika kufuatilia mpito wa kuondokana na nishati ya makaa yamawe ili kusaidia kufanikisha lengo la Bwana Guterres la kuondokana na matumizi ya makaa yam awe katika nchi tajiri ifikapo mwaka 2030 na katika nchi nyingine ifikapo mwaka 2050,” imesema taarifa hiyo. 

Halikadhalika atahakikisha kuwa hatua zozote za kukabili janga la Corona au COVID-19 linazingatia malengo ya mkataba wa Paris. 

Bloomberg ambaye alikuwa meya wa 108 wa jiji la New York, anafahamika kwa utoaji wa misaada na pia harakati za kukabili mabadiliko ya tabianchi na ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha John Hopkins University na shule ya biashara ya Havard.