Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko la ardhi la karibuni limewajengea mnepo Wahaiti

Haiti ni moja ya nchi masikini zaidi duniani ambako wananchi wake wanaishi kwakutegemea misaada kutoka kweney mashirika ya misaada
IFRC
Haiti ni moja ya nchi masikini zaidi duniani ambako wananchi wake wanaishi kwakutegemea misaada kutoka kweney mashirika ya misaada

Tetemeko la ardhi la karibuni limewajengea mnepo Wahaiti

Msaada wa Kibinadamu

Raia wa Haiti ambao waliathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililopiga kusini magharibi mwa nchi mwezi Agosti mwaka huu wameonesha "ustahimilivu na mnepo wa hali ya juu" kwa mujibu wa mfanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM), ambaye amekuwa mstari wa mbele na kuunga mkono juhudi za uokozi.

Joseph Chlela, ambaye anatokea Lebanon, ni mratibu wa masuala ya dharura katika shirika la IOM na amekuwa akifanya kazi katika eneo lililoathirika zaidi na  tetemeko hilo la ardhi.

“Nilifika kutoka Bangladesh wiki mbili tu kabla ya tetemeko la ardhi kupiga Haiti. Ninashukuru kwa uzoefu wangu wa kufanya kazi katika hali za shida, ambao umenisaidia kuchukua hatua za dharura mara tu baada ya tetemeko la ardhi kupiga Haiti.”

Hatua ya kwanza muhimu zaidi ni kudhibiti dharura. Niliweka pamoja timu ya kuchukua hatua inayofanya kazi kwa karibu na mashirika ya serikali na washirika wa ndani.  

Timu hiyo ilipelekwa haraka katika maeneo yaliyoathirika zaidi kufanya tathmini ya haraka ya uharibifu na mahitaji na kuanza kusambaza vifaa visivyo vya chakula na vifaa vya kusaidia makazi kama vile mahema, taa zinazotumia nishati ya  jua au Sola pamoja na vifaa vya usafi na vyombo vya jikoni.

Hatua za haraka ni muhimu sana ili kupunguza uharibifu na majeruhi na kutoa usaidizi wa haraka kwa wale wasio na paa la kulala.

Joseph Chlela mratibu wa misaada ya dharura wa IOM
IOM/Monica Chiriac
Joseph Chlela mratibu wa misaada ya dharura wa IOM

Hali ya usalama ni tete

Changamoto kuu zimekuwa za vifaa na kuhusishwa na hali tete ya usalama nchini Haiti, ambayo imefanya kuwa vigumu zaidi kuwafikia watu hao wanaohitaji msaada.

Janga la COVID-19 limefanya kuwa vigumu zaidi kutoa msaada wa kibinadamu.

Jamii nyingi zinaishi katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa ambako kwa kawaida ufikiaji ni mdogo na sasa ni vigumu zaidi kwa sababu ya madaraja na barabara ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi.

Ikiwa watu hawangepokea usaidizi wowote na vifaa kama vile vifaa vya usafi, matukio ya magonjwa ya kuambukiza na yanayosambazwa na maji yangeongezeka sana.

Ukosefu wa makazi pia unahusishwa kwa karibu na ongezeko la hatari ya unyanyasaji wa kijinsia.
Washirika wengine wa serikali na mamlaka za mashinani pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa, likiwemo shirika la kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula duniani WFP, pia wamechangia katika kuchukua hatua za misaada.

“Nimefurahishwa kuona washirika wote, wa ndani na wa kimataifa, wakija pamoja kusaidia wale walioathirika licha ya changamoto lukuki za ugavi. Na inatia moyo kushuhudia mnepo walionao Wahaiti na azma yao ya kukaa katika nyumba zao na kujenga upya vyema zaidi maisha yao.”

IOM imesaidia zaidi ya watu 150,000 kwa makazi na vitu visivyo vya chakula na nadhani watu ambao tumewasaidia, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya mbali sana, walishukuru na labda hata kushangazwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na shirika la IOM.

“Cha muhimu hap ani kwamba kama watu walio msitari wa mbele IOM imewapa matumaini watu wa Haiti kwamba hawajasahaulika wakati walio na uhitaji zaidi."