Skip to main content

Nusu ya watu Afghanistan wanakabiliwa na njaa kali:WFP/FAO

Familia ikirejea nyumbani baada ya kupokea mgao wa chakula cha WFP katika eneo la usambazaji nje kidogo ya Herat, Afghanistan.
© WFP/Marco Di Lauro
Familia ikirejea nyumbani baada ya kupokea mgao wa chakula cha WFP katika eneo la usambazaji nje kidogo ya Herat, Afghanistan.

Nusu ya watu Afghanistan wanakabiliwa na njaa kali:WFP/FAO

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP na la chakula na kilimo FAO yametoa ombi la msaada wa haraka ili kunusuru maisha ya mamilioni ya watu Afghanistan wakati huu taifa hilo likiwa ni moja ya mataifa yenye mgogoro mkubwa wa chakula.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, mashirika hayo yamesema zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote nchini Afghanistan ambayo ni sawa na watu milioni 22.8 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kuanzia Novemba, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya uainishaji wa hali ya uhakika wa chakula (IPC) iliyotolewa na kikundi cha uhakika wa chakula na kilimo cha Afghanistan, kinachoongozwa na FAO na WFP.

Sababu mchanganyiko kama za ukame, mizozo, COVID-19 na changamoto za uchumi, zimeathiri sana maisha, na uwezo wa watu kuishi, na hasa upatikanaji wa watu chakula.  

Matokeo ya ripoti hiyo yanakuja wakati baridi kali ya Afghanistan inaanza ikitishia kukata maeneo ya nchi hiyo ambayo familia hutegemea sana misaada ya kibinadamu kuishi katika miezi ya baridi kali.

Hali halisi ya njaa

IPC imebaini kwamba mtu mmoja kati ya wawili nchini Afghanistan atakabiliwa na hali mbaya ya chakula kiwango cha daraja la 3 na la 4 na kuishi bila kuwa na uhakika wa chakula kuanzia Novemba 2021 hadi Machi 2022 ambao ndio wakati wa muambo na hivyo kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu kuweza kukidhi mahitaji ya msingi, kulinda uwezo wa kuishi na kuzuia janga la kibinadamu.

Ripoti hiyo ya hali ya uhakika wa chakula Afghanistan pia imeeleza kwamba hii ni idadi kubwa ya watu wasio na uhakika wa chakula kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha miaka 10 katika taifa hilo.

Mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema "Ni jambo la dharura kuchukua hatua kwa haraka na kwa ufanisi kuongeza kasi ya utoaji wetu wa misaada nchini Afghanistan kabla ya majira ya baridi kali kushika kasi na kukata sehemu kubwa ya nchi, na mamilioni ya watu wakiwemo wakulima, wanawake, watoto wadogo na wazee hukabiliwa na njaa kali katikia msimu wa baridi. Ni suala la uhai au kifo. Hatuwezi kusubiri na kuona majanga ya kibinadamu yakitokea mbele yetu  haikubaliki!”

Kwa upande wake mkurugenzi mtendani wa WFP David Beasley ameonya kwamba "Afghanistan sasa ipo katika mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni kama sio mbaya zaidi na uhakika wa chakula umeporomoka kabisa.Msimu huu wa baridi mamilioni ya Waafghani watalazimika kuchagua kati ya uhamiaji na njaa isipokuwa tu kama tutaweza kuongeza msaada wetu wa kuokoa maisha, naendapo uchumi utaweza kufufuliwa. Tunakabiliwa na janga na ikiwa hatutachukua hatua sasa, tutapata maafa mkubwa mikononi mwetu, "

Ameongeza kuwa “Njaa inaongezeka na Watoto wanakufa. Hatuwezi kuwalisha watu kwa ahadi, ahadi za ufadhili lazima zigeuke kuwa fedha na jumuiya ya kimataifa lazima ije pamoja kushughulikia mgogoro huu ambao unakuwa kwa kasi nan je uya uwezo wetu wa kiudhibiti.”

Akina mama na watoto katika kliniki ya lishe inayofadhiliwa na WFP huko Herat, Afghanistan.
© WFP/Marco Di Lauro
Akina mama na watoto katika kliniki ya lishe inayofadhiliwa na WFP huko Herat, Afghanistan.

Njaa inasambaa kuanzia vijijini hadi mijini

Ripoti ya IPC inasema kuna ongezeko la asilimia 37 ya watu wanaokabiliwa na njaa kali tangu tathimini ya mwisho ilipofanyika Afrili 2021.

Miongoni mwa watu walio hatarini ni Watoto milioni 3.2 wa chini ya umri wa miaka mitano ambao wanatarajiwa kuugua utapiamlo mkali ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Ripoti imeongeza kuiwa kwa mara ya kwanza wakazi wa mijini wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula kwa kiwango saw ana wale wa jamii za vijijini.

Katika maeneo ya vijijini athari mbaya za awamu ya pili ya ukame katika kipindi cha miaka 4 zinaendelea kuathiri uwezo wa watu milioni 7.3 kuishi, ambao wanategemea kilimo na ufugaji ili kuweza kuishi.

Katikati ya janga hili la ukame unaozidi kuwa mbaya, FAO inahitaji dola milioni 11.4 kwa ajili ya ufadhili wa dharura wa kusaidia masuala ya kibinadamu na inatafuta dola zingine milioni 200 zaidi kwa ajili ya msimu wa kilimo hadi 2022.  

FAO sasa inasambaza vifurushi vya kilimo cha ngano, pamoja na mbegu za hali ya juu, zinazotolewa na mbolea, mbolea na mafunzo.  

Kampeni hii inatarajiwa kufaidi watu milioni 1.3 katika mikoa 27 kati ya 34 ya nchi hiyo katika wiki zijazo.