Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya watu wa Syria wanakabiliwa na njaa wakati vita ikiwa ni mwaka wa 12 sasa: WFP

WFP inatoa chakula kwa familia mjini Aleppo zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi la hivi karibuni nchini Syria.
© WFP/Hussam Al Saleh
WFP inatoa chakula kwa familia mjini Aleppo zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi la hivi karibuni nchini Syria.

Nusu ya watu wa Syria wanakabiliwa na njaa wakati vita ikiwa ni mwaka wa 12 sasa: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Wastani wa mshahara wa kila mwezi nchini Syria kwa sasa unakidhi takriban robo tu ya mahitaji ya chakula ya familia, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula  duniani WFP, likiangazia hitaji la dharura la kuongezwa msaada wa kibinadamu wakati nchi hiyo ikikabiliana na athari mbaya za matetemeko ya ardhi ya hivi karibuni na miaka 12 ya vita.

Takriban watu milioni 12.1 ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya wakazi, kwa sasa hawana uhakika wa chakula na wengine milioni 2.9 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa. Wakati huo huo, takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa utapiamlo unaongezeka, huku viwango vya kudumaa na utapiamlo wa uzazi vikifikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa.

"Mashambulizi ya mabomu, watu kutawanywa, kutengwa, ukame, kuzorota kwa uchumi, na sasa matetemeko ya ardhi ya viwango vya kushangaza. Wasyria wana mnepo mkubwa lakini kuna kiwango cha mengi ambayo watu wanaweza kuhimili, " amesema Kenn Crossley, mkurugenzi wa WFP nchini Syria na kuongeza kuwa  "Ni wakati gani ulimwengu utasema sasa imetosha?"

Kupanda kwa gharama za chakula

WFP inasema matetemeko ya ardhi ya Februari 6 yalikuja wakati bei ya chakula nchini Syria tayari ilikuwa ikipanda.

Baadhi ya bidhaa za kawaida za vyakula ambazo WFP hutumia kufuatilia mfumuko wa bei za vyakula bei imekaribia kuongezeka maradufu katika kipindi cha miezi 12 na ni ghali mara 13 zaidi ya miaka mitatu iliyopita na ongezeko hilo la bei linatarajiwa kuendelea.

Matetemeko ya ardhi ya hivi karibuni yamethibitisha hitaji la dharura la kuongezeka kwa usaidizi wa kibinadamu nchini Syria, sio tu kwa watu waliokumbwa na matetemeko ya ardhi, lakini pia kwa wale ambao tayari walikuwa wakipambana na kupanda kwa bei ya chakula, adha ya mafuta, na mfululizo wa majanga ya hali ya hewa.

Bei za vyakula na mafuta ziko juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika muongo mmoja baada ya miaka mingi ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya sarafu.

Viwango vya kudumaa miongoni mwa watoto vimefikia asilimia 28 katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na utapiamlo wa wakati wa uzazi sasa ni asilimia 25 kaskazini-mashariki mwa Syria.

Nchi iliyokuwa ikijitosheleza kwa uzalishaji wa chakula sasa inashika nafasi ya kati ya nchi sita zenye uhaba mkubwa wa chakula zaidi wa duniani, zikiwa na zikitegemea kwa kiasi kikubwa kuagiza chakula kutoka nje.

Miundombinu iliyoharibiwa, gharama ya juu ya mafuta na hali ya ukame imepunguza uzalishaji wa ngano wa Syria kwa asilimia 75.

Msaada wa WFP

WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu milioni 5.5 kote nchini Syria, ukijumuisha mchanganyiko wa ugawaji wa chakula, programu za lishe, milo shuleni, usaidizi wa fedha taslimu, na msaada kwa ajili ya kujikimu kimaisha, mnepo na hifadhi ya jamii. Tangu tetemeko la ardhi lilipotokea kaskazini mwa Syria, WFP imewafikia watu milioni 1.7 walioathiriwa na tetemeko la ardhi, ikiwa ni pamoja na watu ambao tayari wanafaidika na msaada wa chakula wa kila mwezi.

Lakini uhaba wa fedha kwa WFP nchini Syria unatishia kupunguza msaada huo, wakati ambapo watu wanauhitaji zaidi.

WFP inahitaji haraka kimakiasi cha dola milioni 450 ili kuendelea kusaidia zaidi ya watu milioni 5.5 kote nchini Syria kwa kipindi kilichosalia cha mwaka 2023.

Hii inajumuisha dola milioni 150 za kusaidia watu 800,000 walioathiriwa na tetemeko la ardhi kwa muda wa miezi sita.

Bila fecha WFP itapunguza msaada

Bila rasilimali za kutosha, WFP imeonya kwamba italazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu inaowahudumia kuanzia Julai mosi mwaka huu na kuendelea, na kuwaacha mamilioni ya watu wakiwa katika uhitaji mkubwa bila msaada wa chakula.

“Dunia sasa imetusahau. Hilo ndilo tunalosikia kutoka kwa Wasyria wengi, na ni ukumbusho tosha kwamba tunahitaji kufanya  jitihada zaidi,” amesema mkurugenzi wa WFP wa Kanda ya Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki Corinne Fleischer.

Ameongeza kuwa "Tunahitaji fedha ili kuendelea kutoa msaada wa chakula kwa mamilioni ya familia hadi Wasyria waweze kujilisha tena wenyewe."

Pamoja na kutoa msaada wa haraka wa chakula, WFP inashughulikia kutafuta suluhu za muda mrefu ili kuzisaidia jamii nchini Syria kutotegemea msaada wa moja kwa moja wa chakula.

Kote Syria, WFP inaunga mkono ukarabati wa mifumo ya kilimo ya umwagiliaji, viwanda vya kusaga, biashara ya mikate na masoko.

Miradi kama hiyo shirika hilo linasema huleta faida kubwa kwenye uwekezaji ikilinganishwa na usambazaji wa msaada wa chakula asilia.

Kwa mfano, kila dola 1 iliyowekezwa katika ukarabati wa viwanda vya kuzalisha mikate au mifereji ya umwagiliaji inaweza kupunguza gharama ya kila mwaka ya msaada wa jumla wa chakula kwa zaidi ya Dola 3.